Mahakama ya Gabon 'yahalalisha' ushindi wa Bongo
24 Septemba 2016Uamuzi huo ambao ulisomwa saa 7:00 usiku wa kuamkia leo Jumamosi (24 Septemba) katika chumba cha mahakama ambacho takribani kilikuwa kitupu, ulizua wasiwasi wa kuanza upya kwa ghasia ambazo zilizuka baada ya Tume ya Uchaguzi kumtangaza Bongo kupata ushindi finyu dhidi ya Ping mwezi uliopita.
Mara tu baada ya uamuzi huo wa mahakama, Bongo alilihutubia taifa akirejelea wito wake wa kuwepo kwa mdahalo wa wazi wa kisiasa ili kuwaleta pamoja wasaidizi na wapinzani wake kufanya kazi pamoja kwa maslahi ya nchi.
"Tunapomaliza uchaguzi na familia zikalazimika kuomboleza vifo vya wapendwa wao, maana yake ni kuwa tumeisaliti demokrasia," aliwaambia wafuasi wake muda mchache kabla ya hotuba yake kuingiliwa na wimbo wa taifa.
Uamuzi wa Mahakama ya Katiba
Katika shauri lake mahakamani, Ping alituhumu kuwepo kwa wizi wa kura kwenye jimbo la Haut-Ogooue, ambako Bongo alitangaziwa kupata asilimia 95 ya kura huku idadi ya waliojitokeza wakiwa asilimia 99.9.
Waangalizi wa Umoja wa Ulaya ulielezea kuwa kulikuwa na mambo mengi yasiyo ya kawaida kwenye matokeo ya jimbo hilo. Hata hivyo, mahakama ilikataa kuzipokea nakala za matokeo ya kura yaliyokusanywa na timu ya Ping kama ushahidi, ikisema nyingi zao hazikuwa halali.
Badala yake, timu ya wanasheria wa Bongo iliwasilisha ushahidi mahakamani kukataa madai ya timu ya Ping, ikidai ni Ping mwenyewe ndiye aliyechochea wizi wa kura.
Mahakama hiyo ilifuta matokeo ya vituo 21 vya kura katika mji mkuu, Libreville, kutokana na makosa mbalimbali ya kisheria. Matokeo ya uamuzi wa mahakama sio tu yamekuwa ni kulihalalisha tangazo la ushindi wa Bongo lililotolewa na Tume ya Uchaguzi mwezi uliopita, bali pia kuuongeza ushindi huo.
Kwa mujibu wa mahakama, ushindi wa Bongo umevuuka kutoka asilimia 49.85 wa awali hadi 50.66 katika matokeo ya mwisho yaliyotangazwa jana.
Timu ya mawakili wa Ping haikuwepo mahakamani wakati uamuzi huo ukitolewa.
Ping hataki mazungumzo na Bongo
Kuna uwezekano mdogo sana kwa Ping, ambaye anadai alishinda uchaguzi huo, kukubali kuingia kwenye mazungumzo na Bongo, ambaye kifamilia ni shemegi yake. Mke wa kwanza wa Ping na ambaye amezaa naye mtoto mmoja ni dada yake Bongo.
Shirika la habari la AFP linaripoti kwamba Ping mwenyewe aliangalia televisheni wakati uamuzi huo wa mahakama ukisomwa akiwa na wafuasi wake.
"Taasisi za nchi zinazotenda mambo kama haya, ni jambo la huzuni sana," alisema mmoja wa wafuasi hao, Olivier. "Daima mwenye nguvu ndiye mshindi. Sauti ya umma imekataliwa."
Vikosi vya usalama vilisambazwa kwenye maeneo kadhaa ya mji mkuu, Libreville, siku kadhaa kabla ya uamuzi huu, na usiku wa Ijumaa vikosi zaidi vikaongezwa.
Waziri wa mawasiliano alimuonya Ping siku ya Jumatano kwamba angelikamatwa endapo ghasia zingezuka baada ya uamuzi wa mahakama.
Katika ghasia za mwezi uliopita, watu sita waliuawa, kwa hisabu ya serikali, huku maeneo kadhaa kwenye mji mkuu, Libreville, na miji mingine yakiharibiwa.
Upinzani unadai kwenye machafuko hayo, idadi ya waliopoteza maisha inapindukia 100 na umetoa wito wa uchunguzi huru.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Sudi Mnette