Mahakama ya Haki yaanza kusikiliza kesi dhidi ya Ujerumani
8 Aprili 2024Haya ni kwa kuzingatia madai kwamba Berlin inasaidia vitendo vya mauaji ya kimbari na kukiuka sheria ya kimataifa ya kiutu katika vita kati ya Israel na Hamas.
Nicaragua iliyowasilisha kesi hiyo inadai kwamba hatua ya Ujerumani kuipatia Israel msaada wa kisiasa, kifedha na kijeshi na kuondoa ufadhili kwenye shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Palestina, UNRWA inaashiria wazi kwamba wanaratibu mauaji ya kimbari na kwa namna yoyote ile wameshindwa kutimiza wajibu wa kufanya kila linalowezekana kuzuia mauaji ya kimbari.
Licha ya walengwa wakuu kwenye kesi hiyo kuwa ni Ujerumani, lakini inailenga pia kampeni ya kijeshi ya Israel katika Ukanda wa Gaza, ingawa si moja kwa moja.
Ujerumani inakana madai ya Nicaragua ikisema haijakiuka mkataba wa kuzuia mauaji ya Kimbari au sheria ya kimataifa inayohusu masuala ya kiutu, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, sebastian Fischer, siku ya Ijumaa.