1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC kutoa hukumu nyingine dhidi ya Jean-Pierre Bemba

Isaac Gamba
22 Machi 2017

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC hii leo inatarajiwa kutoa hukumu dhidi ya Makamu wa Rais wazamani  katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  Jean- Pierre Bemba pamoja na washirika wake wanne.

Niederlande Kongo Jean-Pierre Bemba Gombo wegen Kriegsverbrechen in Den Haag verurteilt
Picha: picture-alliance/dpa/EPA/M. Kooren

Waendesha mashitaka katika mahakama ya ICC wamependekeza kifungo cha miaka minane dhidi ya  Bemba ambaye tayari anakabiliwa na kifungo cha miaka 18 alichohukumiwa na mahakama hiyo kutokana na vitendo vya ukatli vilivyofanywa na wanajeshi waliokuwa wakimuunga mkono katika Jamhuri ya Afrika ya Kati katika kipindi cha kati ya mwaka 2002 na 2003.

Mmoja wa wanaharakati wa masuala ya kisheria kutoka taasisi moja ya kimataifa inayohusika na ushauri katika masuala ya kisheria, Mariana Pena amesema adhabu ya aina hiyo iwe ndogo au kubwa itakuwa fundisho kuhusiana na uzito wa kosa lenyewe.

Waendesha mashitaka wa mahakama ya ICC wamependekeza Jean Pierre Bemba mwenye umri wa miaka 54 ahukumiwe kifungo kingine cha ziada licha ya kifungo kingine cha awali.

Waendesha mashitaka hao pia wamependekeza majaji wa mahakama ya ICC kutoa adhabu ya kifungo cha miaka minane gerezani dhidi ya mwanasheria wa Bemba Aime Kilolo pamoja na mwanasheria wake mwingine Jean-Jacques Mangenda ambaye waendesha mashitaka  wamependekeza kifungo cha miaka saba dhidi yake, miaka mitano  kwa  shahidi wa Bemba Narcisse Arido na miaka mitatu jela kwa mmoja wa wabunge nchini humo Fidele Babala.

Mahakama ya ICC ilimtia hatiani Bemba kwa kosa hilo Oktoba mwaka 2016

Narcisse Arido,Shahidi wa upande wa utetezi katika kesi inayomkabili Jean-Pierre Bemba:Picha: picture-alliance/dpa/M. Kooren

Kiongozi huyo wazamani wa waasi pamoja na washirika wake wanne walitiwa hatiani Oktoba mwaka jana kwa kosa la kutoa rushwa kwa mashahidi kuhusiana na kesi ya  awali iliyokuwa ikiwakabili kwa lengo la kuwashawishi kupotosha ukweli na hukumu hii ni ya kwanza ya kipekee katika mahakama hiyo ya ICC.

Waendesha mashitaka wanasema mbabe huyo wazamani wa kivita aliratibu mtandao maalumu kwa ajili ya kutoa rushwa kwa mashahidi 14 wa kesi hiyo akiwa na lengo la kuwashawishi kusema uongo kuhusiana na mashitaka yaliyokuwa yakimkabili.

Mahakama hiyo ya ICC iliyoanzishwa mwaka 2002 kushughulikia makosa yanayohusiana na uhalifu wa kivita imekuwa ikijitahidi kwa kiwango cha hali ya juu kujaribu kuwalinda mashahidi wasiweze kuingiliwa kwa njia yoyote ile.

Hukumu hii inaelezwa kuwa itakuwa fundisho kwa watuhumiwa wengine ili wasirudie kosa kama hilo  kutokana na ukweli kuwa hii si mara ya kwanza kwa  tuhuma kama hizo zinazohusiana na mashahidi katika mahakama  ya ICC kujaribu kushawishiwa kwa njia moja ama nyingine ili wapotoshe ukweli.

Mahakama ya  ICC ililazimika kutupilia mbali mashitaka yaliyokuwa yakimkabili Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na Makamu wake William Ruto baada ya kuthibitika kuwa mashahidi katika kesi hiyo walitishwa. 

Mwandishi: Isaac Gamba/afpe

Mhariri      :Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW