Mawakili wasema hakuna ushahidi wa kumhusisha Ruto
14 Januari 2016Ruto ambaye anahudhuria kikao cha kesi hiyo ya The Hague,anakabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu kutokana na vita vya baada ya uchaguzi wa urais nchini Kenya mwaka 2007 ambapo watu 1,200 waliuawa.
Mahakama ya ICC imekumbana na changamoto kadhaa kwenye kesi za Kenya,kesi ambazo ni miongoni mwa zinazowahusu watu wa ngazi za juu kuwahi kushughulikiwa na mahakama hiyo. Viongozi wa mashtaka waliondoa mashtaka dhidi Rais Uhuru Kenyatta mwaka uliopita kufuatia kile walichokitaja ni kujiondoa kwa mashahidi.
Mawakili wa Ruto wamesema kujiondoa kwa mashahidi 6 wa upande wa mashataka kumewafanya viongozi wa upande huo wa mashtaka kutoa madai yasiyoendana na tuhuma kwamba alishirikiana kuwaondoa wafuasi wa upinzani kwenye makaazi yao.
Wakili asema hakuna ushahidi
Kwa hivyo basi wakili huyo wa Ruto ameongeza kusema kwamba "Msingi wa kesi hii umekwisha".
Khan ameliambia jopo la majaji watatu kwenye kesi hiyo ya kutathmini ikiwa Ruto ana kesi ya kujibu kwa kuhusika kwenye mapigano yaliyotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 hadi 2008 au la, kuwa ushahidi umekosekana kwenye kesi hiyo.
Wakili huyo amesema viongozi wa mashtaka hawadai tena kuwa mikutano ya kupanga ghasia ilifanyika ambapo ufadhili wa kifedha ,kijeshi na kisiasa ulipanga mashambulizi chini ya uongozi wa Ruto.
Ruto mwenye umri wa miaka 49 na mtangazaji Joshua arap Sang mwenye umri wa miaka 40 wanakabiliwa na mashtaka matatu ya uhalifu dhidi ya binadamu ikiwemo mauaji,kuwahamisha watu kwa nguvu na mateso yaliyotokana na machafuko yaliyojiri baada ya uchaguzi uliokumbwa na utata wa mwaka 2007.
Viongozi wa mashtaka walisema wiki hii kuwa bado kuna ushahidi wa kutosha wa kuendelea na kesi hiyo.
Viongozi wa mashtaka wanasema zaidi ya watu 1,300 waliaga dunia na 600,000 wengine kuachwa bila makaazi kwenye mzozo mbaya zaidi kuwahi kutokea kwenye nchi hiyo tangu uhuru 1963.
Endapo madai yanayomkabili Ruto yatatupiliwa mbali hatua hiyo itampa fursa ya kufanya kampeni yake kama mgombea mwenza wa Kenyatta kwenye uchaguzi wa urais mwaka 2017,na kumuweka katika nafasi nzuri ya kuwania urais mwaka 2022.
Waendesha mashtaka wanasema tangu walipioshinda katika uchaguzi wa mwaka 2013 rais Kenyatta na Ruto changamoto zimekuwa zikiiikabili kesi hizo kutokana na mashahidi kupewa vitisho pamoja na kuhongwa.
Licha ya kuundwa miaka 13 iliyopita na kuwawajibisha watu wenye ushawishi mkubwa wanaotekeleza uhalifu wa kimataifa,mahakama hiyo ya ICC imefanikiwa kutoa hukumu mbili pekee kwa gharama ya zaidi ya Uro bilioni moja na imekuwa ikiendelea kujizatiti kuwafikisha watu mashuhuri kwenye mahakama hiyo ya The Hague.Majaji wamewalaumu viongozi wa mashtaka kwa kutegemea sana ushahidi unaotolewa na watu ambao unaweza kukanushwa kirahisi na kupuuza kufanya uchunguzi kikamilifu..
Mwandishi:Bernard Maranga/AFP/Reuters
Mhariri:Yusuf Saumu