1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya ICJ kusikiliza kesi ya Iran dhidi ya Marekani

4 Februari 2021

Mahakama ya juu ya Umoja wa Mataifa imekubali kusikiliza malalamiko ya Iran ya kutaka iondolewe vikwazi ilivyowekewa tena na Marekani wakati wa utawala wa Donald Trump.

Iran | Außenminister Mohammed Dschawad Sarif
Picha: Russian Foreign Ministry Press Office/dpa/picture-alliance

Waziri wa kigeni wa Iran Mohammed Javad Zarif amepongeza uamuzi huo wa Jumatano unaohusu kesi iliyowasilishwa miaka mitatu iliyopita katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) mjini The Hague.

Iran inadai rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, alikiuka makubaliano ya urafiki ya mwaka 1955 kati ya nchi hizo mbili, alipojitoa kwenye makubaliano ya nyuklia. Na baadae Trump aliamrisha kuirudishia tena vikwazo vya kiuchumi Iran.

Soma zaidi: Iran kurutubisha madini ya Uranium kwa asilimia 20

Marekani imesema mahakama ya ICJ ya mjini The Hague haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo. Na imesisitiza kwamba vitendo vya Iran vinahatarisha usalama wa wa kimataifa. Hata hivyo majaji katika mahakama hiyo wameyakataa madai yote ya Marekani.

Rais wa ICJ Abdulqawi Ahmed Yusuf amesema mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza ombi lililowasilishwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani ilijibu kwa kusema imesikitishwa sana na uamuzi huo.

Msemaji wa serikali ya Marekani Ned Price, amesema baadae watatoa maelezo zaidi juu ya kwanini madai ya Iran hayana maana.

Mjaaji katika mahakama ya ICJ, The HaguePicha: picture-alliance/dpa/epa/J. Lampen

Iran yautaka Umoja wa Ulaya kuwa mpatanishi 

Makubaliano ya nyuklia yaliyosainiwa mwaka 2015 yaliitaka Iran kupunguza harakati za kuimarisha mpango wake wa nyuklia, na kuwaruhusu nchini mwake wachunguzi wa kimataiga kwa ukaguzi. Kwa kufanya hivyo mataifa ya Magharibi yalikubali kuiondolea Iran vikwazo vya kiuchumi iliyokuwa imewekewa kwa miaka mingi.

Lakini baada ya Trump kujitoa kwenye makubaliano hayo aliiwekea tena vikwazo ambayo Iran inadai vimesababisha ugumu wa maisha ulioathiri mamilioni ya raia wake.

Huu ni ushindi wa pili katika kesi hiyo. Mnamo mwaka 2018, mahakama ya ICJ iliiamrisha Marekani kuilegezea vikwazo Iran katika misaada ya kibinadamu.

Kufuatia uamuzi huo wa ICJ, waziri wa kigeni wa Iran ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba Iran daima imekuwa ikiheshimu sheria za kimataifa, na umefika wakati kwa Marekani nayo kutimiza wajibu wake.

Makubaliano ya nyuklia ya 2015 yalihusisha wanachama watano wa kudumu wa Baraza ya Usalama la Umoja wa Mataifa ambao ni Uingereza, China, Ufaransa, Urusi na Ujerumani.

Rais mpya wa Marekani Joe Biden amesema anaunga mkono Marekani kurudi katika makubaliano hayo lakini ameitaka Iran kubadilisha msimamo wake uliochukuwa baada ya Trump kujitoa na kuiwekea vikwazo.

Na Zarif ameiutaka Umoja wa Ulaya kuwa mpatanishi kati ya Iran na Marekani.

Vyanzo: afp, rtre