Mahakama ya Iran yaapa kuwakabili vikali waandamanaji
5 Januari 2026
Jaji Mkuu nchini humo Gholam-Hossein Mohseni Ejei ameonya kupitia mtandao wa mahakama wa Mizan kwamba waandamanaji wanapaswa kutambua kuwa mahakama hazitaonyesha huruma kama hapo awali na kwamba hakutakuwa na makubaliano zaidi.
Amegusia pia ishara ya mshikamano ulioonyeshwa na waandamanaji wa Marekani na Israel mataifa ambayo ametaja kuwa maadui wa watu wa Iran.
Mapema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmael Baghei ameyashutumu mataifa hayo kwa kutoa matamshi yanayochochea machafuko na ugaidi katikati ya maandamano.
"Vitendo au kauli za waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, na baadhi ya maafisa wenye msimamo mkali wa Marekani, kuhusu masuala ya ndani ya Iran si kitu kingine ila ni uchochezi wa vurugu, ugaidi, na mauaji kwa lugha ya kanuni za kimataifa. Kwa hivyo, tunamshukuru Mungu kwamba watu kama hao hawaaminiwi hapa, na kwamba watu wetu, wala jumuiya ya kimataifa hawatapotoshwa na tabia hii ya kinafiki.”
Rais wa Marekani Donald Trump jana Jumapili alionya kuishambulia vikali Iran ikiwa waandamanaji zaidi watauawa katika machafuko yaliyoitikisa nchi hiyo.