Mahakama Israel: Wanaume wa Kiorthodox waandikishwe jeshini
25 Juni 2024Uamuzi huo wa mahakama umetolewa Jumanne na kuamua kwa kuwa hakuna sheria inayotofautisha kati ya wanafunzi wa seminari ya Kiyahudi na wanafunzi wengine walioandikishwa kujiunga na shule, mfumo wa utumishi lazima wa kujiunga na jeshi la Israel, unapaswa kutumika kwa Waorthodox wote kama vile raia wengine wowote.
Awali, wanaume wa madhehebu ya Kiorthodox walikuwa wanaruhusiwa kutojiandikisha katika utumishi wa kijeshi, jambo ambalo ni lazima kwa wanaume na wanawake wengi wa Israel. Wanaume na wanawake wengi wa Kiyahudi nchini Israeli wanatakiwa kuhudumu kwa lazima jeshini pindi wanapotimiza umri wa miaka 18.
Hayo yanajiri wakati ambapo Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalotoa misaada kwa Wapalestina, UNRWA Philippe Lazzarini akisema kuwa watoto 10 kwa siku wanapoteza mguu mmoja au yote katika vita vya Gaza.
Lazzarini amewaambia Jumanne waandishi habari mjini Geneva huku akizinukuu takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto, UNICEF, akisema idadi hiyo ni takribani watoto 2,000 baada ya zaidi ya siku 260 za vita vya Gaza.
Watoto 14,000 wameuawa tangu vita vilipoanza
''Na kuongezea hili, hii ripoti inasema kwamba watoto 14,000 wameuawa tangu vita vilipozuka. Na unazingatia kwamba kimsingi, kila siku tuna watoto kumi ambao wanapoteza mguu mmoja au miguu yote miwili. Kwa wastani, hii inakupa mtazamo kuhusu aina ya utoto wanaopitia watoto wa Gaza,'' alifafanua Lazzarini.''
Ama kwa upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ametangaza kuwa nchi hiyo itatoa euro milioni 19 kwa ajili ya misaada zaidi ya kwenda Gaza na ameikosoa serikali ya Israel kwa hatua ambazo amesema zinadhoofisha usalama wa muda mrefu wa nchi hiyo.
Baerbock yuko ziarani mjini Jerusalem, kama sehemu ya juhudi za kuzuia vita kati ya Israel na Hamas kutanuka na kuwa mzozo wa kikanda.
Msaada huo utafanya kiasi cha misaada ya kibinadamu iliyotolewa kwenye maeneo ya Wapalestina tangu mwaka uliopita kufikia euro milioni 312, huku sehemu kubwa ya fedha ikienda kwa watu wa Gaza. Msaada wa Ujerumani utazingatia zaidi matibabu na chakula ambavyo vinahitajika kwa haraka zaidi, kuwahamisha majeruhi na wahudumu wa afya, kutoa msaada wa kisaikolojia na katika masuala ya usafi.
WHO: Wagonjwa 2,000 washindwa kuondolewa Gaza
Wakati huo huo, Shirika la Afya Duniani, WHO limesema kuwa kufungwa kwa mpaka wa Rafah kati ya Misri na Gaza kumezuia kuhamishwa kwa wagonjwa wasiopungua 2,000. WHO imetoa wito wa kufunguliwa tena kwa Rafah na njia nyingine.
Mwakilishi wa WHO katika Ukingo wa Magharibi, Rik Peeperkorn amesema kabla ya mpaka huo kufungwa, takribani wagonjwa 50 mahututi walikuwa wakiondolewa Gaza kwa siku.
(AFP, AP, DPA, Reuters)