1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Mageuzi ya sheria ya Netanyahu yapingwa Israel

2 Januari 2024

Mahakama ya juu ya Israel imebatilisha sheria ya mageuzi makubwa yenye utata kwenye mfumo wa mahakama iliyosababisha maandamano makubwa dhidi ya serikali ya mseto wa vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia nchini humo.

Israel | Jerusalem | Maandamano dhidi ya mabadiliko ya mfumo wa Mahakama
Maelfu ya raia wa Israel walijiunga na maandamano ya kila wiki dhidi ya mabadiliko ya mfumo wa Mahakama, yaliyogubikwa na mashambulizi ya Hamas mnamo Oktoba 7Picha: Ilia Yefimovich/dpa/picture alliance

Katika kile kinachoonekana kama pigo kubwa kwa serikali ya Israel inayoongozwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, majaji wanane kati ya 15 waliunga mkono hatua ya kuubatilisha uamuzi huo wa sheria iliyopitishwa mwezi Julai na kusema marekebisho hayo ya katiba, yaliinyima mahakama nafasi ya kuchukua hatua dhidi ya maamuzi yasiyofaa, yatakayochukuliwa na serikali, waziri mkuu au wajumbe wengine wa baraza la mawaziri.

Bunge la Israel lapitisha sheria tata ya mageuzi ya mahakama

Wakosoaji wa marekebisho hayo yaliyofanywa na serikali ya siasa kali za mrengo wa kulia wanasema mabadiliko hayo yangeliweza kuchochea ufisadi na uteuzi wa kiholela katika nyadhifa muhimu serikalini.

Uamuzi huu pia ni pigo la moja kwa moja kwa Netanyahu, ambaye tangu Oktoba 7 umaarufu wake umekuwa ukishuka katika kura za maoni zinazofanyika. Wengi wa wakosoaji wake wamekasirishwa na hatua yake ya kutowajibika kwa shambulizi la kundi la Hamas kusini mwa Israel ambako watu 1,200 waliuwawa.

Netanyahu asitisha mpango tata wa mageuzi ya mahakama

Kabla ya hapo wakosoaji hao walihoji kuwa marekebisho hayo yatahujumu demokrasia ya Israel kwa kuondoa uwezo wa kuidhibiti ofisi ya waziri mkuu, huku serikali ikihoji kuwa inahitaji kuidhibiti idara ya mahakama dhidi ya kuingilia utendaji kazi wa serikali.

Serikali ya Israel yaukosoa uamuzi wa Mahakama

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Picha: Ronen Zvulun/AP Photo/picture alliance

Haijawahi kutokea katika historia ya Israel kwa sheria kubatilishwa na Mahakama ya Juu na kwa sasa taifa hilo litakabiliwa na mgogoro wa kikatiba iwapo serikali ya Netanyahu haitokubali na kuheshimu maamuzi ya Mahakama.

Serikali hiyo iliendelea na mipango yake ya kubadilisha mfumo huo wa sheria za Mahakama licha ya upinzani mkali bungeni. Marekebisho hayo yaliyokuwa muhimu kwa serikali ya Netanyahu tangu ilipoapishwa madarakani mwaka mmoja uliopita, yaliwagawa pakubwa watu wa Israel. Kwa miezi kadhaa, maelfu ya watu waliandamana kuyapinga.

Turk aitaka serikali ya Netanyahu kuwasikiliza waandamaji

Kiongozi wa upinzani nchini Israel Jair Lapid, ameunga mkono hatua ya Mahakama na kusema uamuzi huo umefunga mwaka mgumu uliokuwa na migawanyiko na uliokuwa mbaya katika historia ya Israel. Hata hivyo, baadhi ya maafisa wa serikali wameukosoa na kuhoji kwamba Mahakama ya Juu haina mamlaka ya kubatilisha sheria zilizopitishwa.

Knesset yapitisha sheria tata ya mageuzi ya mahakama

Chama cha Likud chake Netanyuhu pia kimepaza sauti yake juu ya hili na kusema kinasikitishwa na uamuzi uliochukuliwa katikati ya mapambano kati ya Israel na kundi la Hamas. 

dpa