Mahakama ya juu Libya yalifutilia mbali bunge
6 Novemba 2014Waasi wa kiislamu wanaoudhibiti mji mkuu wa Libya Tripoli tangu mwezi Agosti wameupokea uamuzi huo wa mahakama ya juu kwa shangwe na wamefyatua risasi kama ishara ya kusherehekea uamuzi huo ambao hauwezi kukatiwa rufaa.
Mahakama hiyo ya juu iliyoko mjini Tripoli pia imebatilisha marekebisho ya katiba yaliyofanywa na bunge la zamani yaliyopelekea kufanyika kwa chaguzi tarehe 25 mwezi Juni mwaka huu na hivyo kumaanisha uchaguzi huo na matokeo yake hayatambuliki kisheria na yamefutiliwa mbali.
Makundi ya waasi yanadhibiti miji mikuu
Serikali hiyo iliyovunjwa na mahakama inayoongozwa na waziri mkuu Abdullah al Thani ambayo ndiyo inayotambulika rasmi na jumuiya ya kimataifa imekuwa ikiendesha shughuli zake katika mji wa mashariki mwa Libya wa Tobruk ulioko karibu na mpaka na Misri na uongozi huo umepoteza udhibiti wa miji mikuu nchini Libya ambayo iko chini ya waasi wa kiislamu.
Kamati ya bunge kuhusu masuala ya kisheria imeitisha mkutano wa dharura kutathimini uamuzi huo wa mahakama. Mbunge mmoja wa bunge hilo la Tobruk Issam al Jehani ameandika katika ukurasa wake wa facebook kuwa wabunge hawatatambua uamuzi uliofikiwa kwa mtutu wa bunduki.
Mbunge mwingine Abubakar Baeira ameutaja uamuzi huo kuwa wa kisiasa na kuongeza utatoa nafasi kwa taifa hilo kugawanyika.Hata hivyo wakili Abdel Rahman amesema uamuzi huo unamaanisha walibya wanaanza upya
Bunge la Tobruk ndilo la pili kuchaguliwa tangu kung'olewa madarakani na kuuawa kwa Rais Moammar Gaddafi mwaka 2011.Tangu wakati huo,viongozi wa Libya wamejaribu kurejesha uthabiti nchini humo bila mafanikio kutokana na kitisho cha waasi wenye nguvu waliosaidia kumng'oa madarakani Gaddafi ambao wanaidhibiti miji muhimu.
Mapigano yanaendelea Benghazi
Hayo yanakuja huku kukiripotiwa mapigano makali kati ya wapiganaji wanaoiunga mkono serikali na waasi wa kiislamu katika mji wa Benghazi ambapo kiasi ya watu thelathini wameuawa katika kipindi cha siku tatu zilizopita.
Walioshuhudia mapigano hayo wamesema ndiyo mabaya zaidi tangu mkuu wa zamani wa jeshi jenerali Khalifa Haftar kuanzisha mapigano yanayoungwa mkono na serikali dhidi ya wanamgambo mwezi uliopita.
Wakati huo huo, watu waliokuwa na silaha walikishambulia kiwanda kikubwa cha mafuta cha El Sharara jana na kusababisha kufungwa kwa kiwanda hicho, hilo likiwa pigo jingine kwa sekta ya nishati ya nchi hiyo ambayo imetatizika kuzalisha mafuta.
Nchi za magharibi na nchi jirani na Libya zinahofia kuwa taifa hilo mwanachama wa jumuiya ya nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani OPEC linaelekea kutumbukia katika vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe.
Mwandishi:Caro Robi/Reuters/afp
Mhariri: Yusuf Saumu