1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAsia

Mahakama ya Katiba Korea Kusini kuamua hatma ya Rais Yoel

16 Desemba 2024

Mahakama ya Katiba ya Korea Kusini imeanza leo kuupitia uamuzi wa Bunge wa kumwondoa madarakani Rais Yoon Suk Yeol kutokana jaribio lake la kuiweka nchi hiyo chini ya sheria ya kijeshi mnamo wiki mbili zilizopita.

Rais aliyeondolewa madarakani na Bunge nchini Korea Kusini, Yoon Suk Yeol
Rais aliyeondolewa madarakani na Bunge nchini Korea Kusini, Yoon Suk Yeol.Picha: South Korean Presidential Office/Handout/Yonhap/AFP

Majaji wote sita wa mahakama hiyo wanahudhuria mkutano huo wa kwanza juu ya uamuzi wa bunge wa kumwondoa Rais Yeol ambao ulipitishwa siku ya Jumamosi chini ya uongozi wa vyama vya upinzani.

Mahakama hiyo inao muda wa hadi miezi sita kutoa uamuzi wa iwapo Rais Yeol atavuliwa rasmi madaraka yake au kumrejesha mamlakani kuendelea kuliongoza taifa hilo.

Iwapo ataondolewa madarakani, uchaguzi mpya unapaswa kuitishwa ndani ya kipindi cha miezi miwili. Kufuatia kura ya bunge na mchakato wa mahakama, Rais Yeol,  amewachia madaraka kwa muda na serikali ya nchi hiyo inaongozwa na Waziri Mkuu Han Duck-sooy.

Wakati huo huo shirika la habari la Korea Kusini, Yonhap limeripoti kwamba wachunguzi nchini humo wanapanga kumhoji Rais Yeol mnamo wiki hii kuhusiana na jaribio lake lililoshindwa la kutangaza sheria ya kijeshi.

Duru zinasema mahojiano hayo huenda yafanyika siku ya Jumatano. Yeol pia bado yuko chini ya kizuizi cha kusafiri nje ya nchi wakati uchunguzi dhidi yake unaendelea.

Yumkini Rais Yeol na maafisa wengine wakashtakiwa kwa uasi dhidi ya dola 

Bunge la Korea Kusini.Picha: Woohae Cho/Pool Photo/AP/picture alliance

Kuna uwezakano kwamba Yeol na maafisa kadhaa waandamizi watakabiliwa na mashtaka ya uasi dhidi ya dola kutokana na tangazo la kiongozi huyo la tarehe 3 Disemba.

Waendesha mashtaka wamesema walikwishamwita mara ya kwanza kiongozi huyo kwa mahojiano lakini "amekataa kuitikia mwito huo" na sasa watatuma mwito mwingine.

Maandamano makubwa dhidi ya Yoon, pamoja na mikusanyiko midogo inayomuunga mkono, vimetikisa mji mkuu wa Korea Kusini, Seoul, tangu amri yake ya sheria ya kijeshi.

Waandamanaji katika kambi zote mbili wameapa kuendeleza shinikizo huku Mahakama ya Katiba ikisubiriwa kuamua hatma ya Yoon.

Hapo jana Jumapili, Polisi waliwakamata wakuu wa sasa na wa zamani wa Kamandi ya Ujasusi ya Ulinzi kuhusiana na madai ya uasi, Yonhap iliripoti.

Waendesha mashtaka nao wamesema  walikuwa wakitafuta hati ya kukamatwa kwa mkuu wa Kamandi Maalum ya Jeshi la Vita Kwak Jong-keun. Taarifa hizo ni kulingana na shirika la habari la Yonhap.

Kwak anatuhumiwa kutuma wanajeshi wa kikosi maalum bungeni wakati wa tangazo la sheria ya kijeshi lilipotolewa, hali iliyozusha makabiliano makubwa kati ya wanajeshi na wafanyakazi wa bunge.

Mkuu wa chama cha Rais Yeol kujiuzulu huku Korea Kaskazini ikitupa kijembe

Mkuu wa chama tawala cha Yoon People Power Party (PPP), ambaye hajahusishwa na tangazo la sheria ya kijeshi na ameonyesha kuunga mkono rais Yeol kuondolewa madarakani, amesema mapema leo kwamba atajiuzulu wadhifa wake.      

Maandamano ya umma nchini Korea Kusini kufuatia tangazo la Rais Yeol la sheria ya kijeshi. Picha: Lee Jin-man/AP/picture alliance

"Ninaomba radhi kwa watu wote ambao wameteseka kutokana na tukio la tangazo la sheria ya kijeshi," Han Dong-hoon aliuambia mkutano wa waandishi wa habari huko Seoul.

Vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini leo Jumatatu vimeshambulia Rais wa Korea Kusini aliyeondolewa madarakani Yoon Suk Yeol vikimtaja kuwa "kiongozi wa uasi". Hayo yalikuwa matamshi ya kwanza tango Yeol alipoondolewa madarakani

Serikali mjini Pyongyang imejizuia kutia neno katika msukosuko wa kisiasa wa Korea Kusini, ambao ulifikia kilele siku ya Jumamosi pale bunge la nchi hiyo lilipopiga kura ya kumwondoa madarakani Rais Yeol kwa "uasi".

Shirika la Habari la Korea Kaskazini (KCNA) liliripoti kuwa Yoon amejaribu kuepusha zahma ya kile limekitaja kwua "tangazo la kipumbavu la sheria ya kijeshi" kwa vyama vya upinzani.

"Uchunguzi dhidi ya kibaraka Yoon Suk Yeol, kiongozi wa uasi, na washirika wake unaendelea," limeripoti shirika la KCNA ilisema.

Vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini mara nyingi huwataja viongozi wa Korea Kusini kuwa "kibaraka" wa mshirika wake wa jadi, Marekani.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW