1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama Kenya yabariki jeshi kutuliza ghasia mtaani

28 Juni 2024

Mahakama nchini Kenya imeidhinisha uamuzi wa kutuma jeshi kukabiliana na maandamano ya kuupinga muswada wa fedha wenye utata ambao serikali imeahidi kuuondoa, huku vijana wa Kenya sasa wakilenga kukabiliana na ufisadi.

Vokosi vya jeshi la Kenya vikishika doria  Nairobi, Kenya Alhamisi, Juni 27, 2024.
Vokosi vya jeshi la Kenya vikishika doria Nairobi, Kenya Alhamisi, Juni 27, 2024.Picha: Brian Inganga/AP/dpa

Mahakama nchini Kenya imeidhinisha uamuzi wa kutuma jeshikuimarisha juhudi za polisi, huku maandamano ya kuupinga muswada wa fedha wenye utata ambao serikali imeahidi kuuondoa, yakiendelea.

Baada ya mafanikio ya kushangaza ya kuilazimu serikali ya Kenya kusitisha uidhinishaji wa muswada wa fedha wa kuongeza kodi ya dola bilioni 2.7, wanaharakati vijana wa Kenya wanaweka mtazamo wao juu zaidi, wakilenga sasa kukabiliana na rushwa na ufisadi uliokita mizizi nchini humo.

Huku magari ya kijeshi ya kivita yakionekana kwenye miji, mahakama ilitoa uamuzi jana jioni kwamba ilikuwa halali kwa bunge la Kenya kuidhinisha kutumika kwa majeshi kutuliza vurugu wakati wa maandamano ambayo polisi hawajaweza kuyadhibiti. 

Soma pia: Waandamanaji kadhaa wauwawa Kenya

Mahakama ilikataa ombi lililowasilishwa mahakamani na chama cha mawakili cha Kenya kikipinga hatua iliyochukuliwa na mahakama. Akitoa uamuzi huo, Jaji Lawrence Mugambi pia alionya kuhusu "mwenendo hatari" ambao unaweza kusababishwa na utumiaji wa jeshi la nchi, ikiwa ni pamoja na kuwatisha watu, kuwazuia raia kuandamana ambayo ni haki yao, na pia kuweka mgawanyiko kati ya jeshi na raia.

Maafisa wa polisi wa Kenya na maafisa wa usalama wakilinda Bunge la Kenya huku waandamanaji wakijaribu kuvamia jengo wakati wa maandamano ya kupinga muswada wa sheria ya fedha wa 2024 katikati mwa jiji la Nairobi, Juni 25, 2024.Picha: LUIS TATO/AFP

Hali iliyoipelekea serikali kugeukia msaada wa jeshi

Kwa hiyo jaji Mugambi ameiagiza serikali ya Kenya, "kutoa taarifa sahihi katika muda wa siku mbili kuhusu upeo na muda wa operesheni hiyo ya majeshi".

Siku ya Jumanne, mamia ya waandamanaji walivamia bunge na kuchoma moto sehemu ya jengo hilo. Hata hivyo, Jaji Lawrence Mugambi pia alionya kuhusu "mwenendo hatari" ambao unaweza kusababishwa na jeshi la nchi. 

Hali ilikuwa ya wasiwasi jijini Nairobi hapo jana wakati waandamanaji walipokuwa wakipanga kuandamana hadi Ikulu, makao makuu ya Rais wa Kenya William Ruto, lakini hawakuweza kufanya hivyo kwani polisi na majeshi walifunga barabara za kuingilia humo, na walikuwa wanashika doria katika mji wote mkuu wa Nairobi.

Waandamanaji waliokuwa mijini kwa siku saba mfululizo wanasema kupitishwa kwa muswada wa fedha wa Rais William Ruto siku ya Jumatano ilikuwa tu dalili ya matatizo katika nchi ambayo vijana wengi wanakabiliwa na ukosefu wa ajira licha ya ukuaji mkubwa wa uchumi.

Waandamanaji Kenya ´wamkalia kooni´ Ruto

02:06

This browser does not support the video element.

Jackson Wachira mfanyibiashara mjini Nairobi anaitaka serikali kuzingatia sauti ya vijana wa Kenya, "wahusishwe katika mipangilio ya serikali, katika mambo ambayo yanaendelea nchini. Na wasiwadharau vijana kwa sababu wao ndio wana sauti na nguvu ya kufanya mambo".

Soma pia: Gachagua: Idara ya Ujasusi yaifelisha serikali ya Kenya

Kihistoria, maandamano nchini Kenya yamekuwa yakiongozwa na wasomi na wanasiasa na mara nyingi huishia katika kugawana madaraka, mikataba ambayo huzaa manufaa machache kwa waandamanaji.

Waandamanaji sasa wanakabiliwa na changamoto ya kudumisha umoja wakiwa wanafuata malengo yao. Wanapaswa kuamua jinsi ya kujibu mualiko wa rais Ruto wa mazungumzo, ambao rais aliutoa siku ya Jumatano.

Soma: Hali ya utulivu yarudi Nairobi baada ya maandamano

Mwandishi na mwanaharakati Nanjala Nyabola anasema, "wengi wa waliohusika katika maandamano ya hivi karibuni walichochewa na msukumo halali wa kuridhika na utendaji kazi wa serikali."

Nanjala anasema, "hakuna dalili kwamba watakuwa tayari kufanya makubaliano iwapo malalamiko hayo hayatashughulikiwa". Lakini kulingana naye, jinsi harakati hizo zisizo na kiongozi na zinanoenezwa kwa kiasi kikubwa kupitia mitandao ya kijamii, zitaleta mafanikio ni suala la kusubiriwa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW