Mahakama ya Kenya yasimamisha ubinafsishaji
5 Desemba 2023Serikali ya Kenya iliyaorodhesha makampuni 35 kuwa katika mpango wa kubinafsishwa na wiki iliyopita makampuni 11 ikiwemo la mafuta na gesi na lile la uendeshaji shughuli za usafirishaji nishati, yalitangazwa rasmi kuwa katika mchakato wa kuuzwa. Hata hivyo chama kikuu cha upinzani kinachoongozwa na Raila Odinga kiliupinga uamuzi huo mahakamani kikitowa hoja kwamba, hatua ya kuuza makampuni hayo inapaswa kuamuliwa kupitia kura ya maoni kutokana na umuhimu wa kimkakati wa makampuni hayo. Jaji Chacha Mwita wa mahakama kuu jana jioni alitowa uamuzi wa kuusitisha mpango wa serikali akisema hatua hiyo imegusa masuala ya kikatiba na kisheria ambayo ni muhimu kwa umma wa Kenya. Kenya inakabiliwa na matatizo makubwa ikiwemo kupungukiwa na mapato pamoja na kuporomoka kwa thamani ya sarafu yake, mambo ambayo yameifanya kuwaongezea mzigo wa matatizo ya kiuchumi wananchi wake.