1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya kijeshi katika jela la Guantanamo

8 Juni 2009

Gereza la Guantanamo: Mtihani kwa Rais Obama

Mahakama ya kijeshi ya Kimarekani katika Gereza la GuantanaoPicha: AP


Mahakama ya kijeshi ya Marekani huko Guantanamo imefanya kikao chake cha kwanza cha hadharani katika utawala wa rais Barack Obama, ikiichunguza kesi ya raia wa Kanada aliye kijana na anayetuhumiwa kumuuwa mwanajeshi wa Kimarekani huko Afghanistan. Kesi hiyo inaashiria juu ya mitihani ambayo Rais Obama anakabiliana nayo katika kuubadilisha mfumo wa tume za kijeshi, moja kati ya ahadi zake za kutaka kulifunga gereza la Guantanamo..


Katika jela la Guantanamo ambalo liko katika kituo cha wanamaji wa Kimarekani, kusini mashariki ya Cuba, bado wanashikiliwa wafungwa 240 wa vita dhidi ya ugaidi. Jaji Patrick Parrish, kanali wa jeshi la Kimarekani, ameamuwa kuzisikiliza hadharani hoja juu ya kesi dhidi ya Omar Khadr, ambaye alikuwa ana umri wa miaka 15 pale alipodaiwa kumuuwa sajenti wa Kimarekani kwa kutumia grenedi.


Katika kesi hiyo, mshtakiwa aliye na umri sasa wa miaka 22 na mzaliwa wa Toronto, Kanada, aliweka wazi kwamba anataka kuachana na timu yake ya mawakili ambao alisema wamekuwa kwa miezi wakiteta kila mmoja dhidi ya mwengine. Alisema hawaamini tena mawakili wake. Jana ilikuwa mara ya kwanza kwa kesi hiyo kusikilizwa tangu Barack Obama atawazwe kuwa rais, na pale aliposhinda mahakamani kwamba kesi zote dhidi ya ugaidi zisimamishwe kwa kipindi cha siku 120. Muda huo ulikwisha mwezi uliopita, lakini upande wa mashtaka umeomba kesi hizo zisimamishwe tena kusikilizwa.


Kepteni John Murphy, mkuu wa upande wa mashtaka, amesema wameomba siku 120 zaidi kwa kesi hizo kuzuiliwa kusikilizwa ili waweze kukamilisha uchunguzi. Na uchunguzi huo unawahusu wafungwqa 11 ambao wamewekwa katika mwenendo wa tume za kijeshi na utawala uliotangulia wa Rais George Bush. Bwana Murphy amesema ombi la kusimamishwa kesi za watu hao lilitolewa ijumaa iliopita, na mahakimu wawili tayari wameshakubali. Kepteni Murphy alisema utawala wa Rais Obama unahitaji kufanya uchunguzi barabara ili uweze kuamuwa katika jukwa gani litakalofaa kwa watu hao kushtakiwa.


Rais Obama alisema mwezi uliopita kwamba atabazibakisha mahakama za kijeshi, mfumo ulioanzishwa na mtangulizi wake, lakini kukiweko baadhi ya mabadiliko. Kutapigwa marufuku kutumia ushahidi uliopatikana kwa kuwalazimisha watuhumiwa, utapunguzwa mtindo wa kutegemea ushahidi wa kusimuliwa na watu wasiohusika na kesi, na wafungwa watakuwa na haki ya kuchaguwa mawakili wao.

Alihoji namna hivi kuhusu jela la Guantanamo:


" Nina imani kwamba tuna nguvu zaidi pale tunapong'ang'ania misingi yetu; tunakuwa dhaifu zaidi pale tunapojitenga na misingi hiyo. Nafikiri kulikuweko kipindi cha wakati, mara baada ya Septemba 11, inafahamika, kwa vile watu walikuwa na woga, ambapo tulidharau mambo mengi na kuchukuwa maamuzi ambayo ni kinyume na namna tulivo kama watu."

Hakimu Parrish aliwakasirikia mahakimu wa kijeshi wa Khadr waliokuweko na akaonya kwamba mtuhumiwa asiwachiwe bila ya kuwakilishwa kisheria hadi pale kesi hiyo itakaposikilizwa tena mwezi July.

Omar Khadr alisema atabakia na wakili wake mkuu, Luteni William Kuebler, ambaye mwaka jana alimuelezea kijana huyo kama mtoto wa miaka 15 aliyekuwa na waoga na alijeruhiwa, mtoto ambaye kwa makosa alihusika katika mzozo wa silaha.

karibu wafungwa 20 watakabiliana na mahakama za kijeshi chini ya kanuni zilizofanyiwa mabadiliko. Waziri wa ulinzi wa Marekani, Robert Gates, amesema karibu washuku 50 hadi 100 wa ugaidi hawatoweza kuachiliwa huru na wala hawawezi kushtakiwa mbele ya mahakama za kijeshi au za kiraia. Wengine wamepangiwa kushtakiwa mbele ya mahakama za Marekani. Wafungwa wengine 50 wamekubaliwa kuhahamishiwa nchi nyingine. Kati yao ni Wachina 176 wenye asili ya Uighur na ambao hawajapatikana na hatia ya ugaidi, lakini bado wako katika jela la Guantanamo. Wa-Uighur hao waliwaambia jana waandishi wa habari waliotembelea jela hilo kwamba wanataka uhuru, na wakauliza iko wapi haki? Utawala wa Rais Obama umeitaka mahakama kuu ya Marekani ilikatae ombi la Wa-Uighur hao kutaka kwenda kuishi Marekani. Pia Wa-Uighur hao hawawezi kurejeshwa kwao China kwa vile huko kuna hatari kwamba watateswa.

Mwandishi: Miraji Othman

Mhariri: Mohamed Abdulrahman




Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW