Mahakama Korea Kusini yatoa hati ya kukamatwa kwa Rais Yoon
31 Desemba 2024Ofisi ya Uchunguzi wa Ufisadi kwa Viongozi wa Vyeo vya Juu imethibitisha kuwa Mahakama ya Wilaya ya Seoul Magharibi iliidhinisha hati iliyoombwa na maafisa wanaochunguza hatua aliyoichukua Yoon ya kutangaza sheria wa kijeshi iliyodumu kwa muda mfupi Desemba 3.
Hii ni mara ya kwanza hati ya kukamatwa imetolewa dhidi ya rais aliyeko madarakani nchini Korea Kusini. Yoon anakabiliwa na uchunguzi wa jinai kuhusu madai kuwa alikuwa kiongozi wa mpango wa uasi.
Uasi ni mojawapo ya mashtaka machache ambayo rais wa Korea Kusini hana kinga. Haijabainika ni lini au ni vipi hati ya kukamatwa kwa Yoon itatekelezwa. Idara ya usalama wa rais ya Korea Kusini imesema katika taarifa kwamba itashughulikia hati hiyo ya kukamatwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria. Mmoja wa mawakili wake amesema kuwa waranti huo ni kinyume cha sheria na batili. Ameongeza kuwa taasisi inayofanya uchunguzi wa kiongozi huyo haina mamlaka ya upelelezi.