Mahakama ya Kyiv yaamuru bilionea Kolomosky kushikiliwa
3 Septemba 2023Mahakama mjini Kyiv Ukraine, imeamuru bilionea Igor Kolomoisky awekwe kizuizini kwa miezi miwili kutokana na tuhuma za udanganyifu na utakatishaji fedha au alipe dhamana yenye thamani ya pesa za Ukraine milioni 509.
Bilionea huyo mwenye umri wa miaka 60, ambaye aliwahi kuwa mshirika wa Rais Volodymyr Zelensky na mmoja wa watu tajiri zaidi Ukraine, alifika katika mahakama akiwa amevalia nguo zenye bendera ya Ukraine.
Shirika la kijasusi la Ukraine SBU limesema Kolomosky alikuwa akishukiwa kuhusika na udanganyifu na kujipatia mali kinyume cha sheria. Mahakama hiyo imeamua kumuweka kizuizini kama hatua ya kujihami. Kolomoisky alimuunga mkono Rais Zelensky wakati alipokuwa mgombea wa Urais mwaka 2019.
Kabla ya kuwa Rais Zelensky alipata umaarufu kama msanii wa vichekesho aliyekuwa akiigiza kwenye televisheni inayomilikiwa na bilionea huyo.