Mahakama ya Pakistan yatoa dhamana kwa Nawaz Sharif
19 Oktoba 2023Kulingana na wakili wake Azam Nazeer, aliyezungumza na waandishi habari nje ya mahakama hiyo ya juu mjini Isamabad, Sharif anapaswa kufika wiki ijayo, mbele ya majaji kuomba kuongezewa kwa muda wa dhamana yake. Umuzi huo sasa utammpa nafasi ya kurejea siku ya Jumamosi mjini Lahore ambayo ni ngome yake ya kisiasa bila ya kukamatwa. Mwenyekiti wa chama chake cha Pakistan Muslim League-Nawaz PML-N Raja Muhammad amesema kurejea kwa Nawaz kunatazamiwa kuwa na maendeleo makubwa.
Shariff aliyewahi kuwa Waziri Mkuu mara tatu Pakistan, aliachiwa kutoka jela kwa dhamana mwaka 2019 kwa lengo la kupata matibabu mini London Uingereza kwa wiki sita, lakini baadae akaamua kutorejea nchini kumaliza kifungo chake.
Sharif achaguliwa waziri mkuu mpya Pakistan baada ya kuondolewa Khan
Nawaz Sharif mmoja ya viongozi walio maarufu katika taifa hilo linalopitia mapinduzi ya mara kwa mara, aliondolewa madarakani mwaka 2017 na kufungwa jela kwa miaka 7, kwa makosa kadhaa ya ufisadi mwaka mmoja baadae. Wakati Sharif akitarajiwa kurejea Pakistan, Mtangulizi wake na hasimu wake wa kisiasa Imran Khan yuko korokoroni baada ya kuondolewa pia katika nafasi yake ya uwaziri Mkuu kwa makosa sawa na ya Sharif.
Mashirika ya kutetea haki za binaadamu yasema kesi dhidi ya viongozi wa kisiasa ni za kubuni
Viongozi hao wote wawili wa zamani, waliondolewa katika nyadhifa zao baada ya kutofautiana na majenerali walio na nguvu katika taifa hilo lililoongozwa kijeshi kwa miongo kadhaa. Mtoto wa kike wa Nawaz Sharif, Maryam Nawaz amesema babaake alitangaza uamuzi wa kurejea nyumbani mwezi Septemba, na anatafuta njia ya kubatilisha hukumu iliyotolewa dhidi yake ili aweze kukiongoza chama chake cha PML-N katika uchaguzi wa kitaifa unaotarajiwa kufanyika Januari mwaka ujao.
Imran Khan kuendelea kukaa jela
Wanasiasa nchini humo hujikuta wamefungamanishwa na kesi za kisheria ambazo mashirika ya kutetea haki za binaadamu yanadai zinabuniwa na jeshi lililo na nguvu ambalo limetawala dola hilo moja mwa moja kwa zaidi ya nusu ya historia yake. Masaibu ya Nawaz yalichukua mkondo mpya wakati kakaake ambaye ndie Waziri Mkuu wa sasa wa Pakistan Shehbaz Sharif, alipoingia madarakani mwaka uliyopita na serikali yake ikafanya mabadiliko ya kisheria ikiwemo kupunguza muda na kuweka uwe wa miaka mitano wa kutowaruhusu wabunge kushiriki uchaguzi.
Aidha wachambuzi wanasema kurejea kwa Nawaz Sharif nyumbani kumetokana na makubaliano yaliyofanywa kati ya jeshi na chama chake lakini serikali ya mpito iliyopo imekanusha madai hayo.
Chanz: afp/reuters