1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya Rufaa Marekani yapinga amri ya Trump

Yusra Buwayhid
10 Februari 2017

Mahakama ya rufaa ya Marekani imepinga amri ya Rais Donald Trump iliyopiga marufuku wahamiaji wa nchi saba za Kiislamu kuingia nchini humo. Trump pia ameukubali msimamo wa China wa kuitaja Taiwan kuwa ni sehemu yake

USA Protestieriende vor dem  9. US Berufungsgericht in San Francisco
Picha: Reuters/N. Berger

Muda mfupi baada ya mahakana kutoa uamuzi wake, Trump aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwa kutumia herufi kubwa, "TUTAKUTANA MAHAKAMANI," na kuongeza "USALAMA WA NCHI YETU UKO HATARINI!"

Na akajibiwa na Jay Inslee, Gavana wa Washington mwanachama wa chama cha Democratic anayeongoza moja ya majimbo yaliyopinga marufuku hiyo. Inslee ameandika "Bwana Rais, tumeshakutana mahakamani, na tumekushinda!"

Waislam nchini Marekani wamefurahishwa na hukumu hiyo ya mahakama ya rufaa.

"Leo ni siku kubwa kwa demokrasia. Mahakama imetuma ujumbe mzito sana kwamba hakuna mtu, pamoja na rais wa Marekani, aliye juu ya sheria. Kimsingi mahakama imesema, katika kukabiliana na hoja ya serikali ya Marekani, kwamba hata rais, matendo yake lazima yapitiwe na mahakama ya shirikisho, hasa pale kunapoulizwa maswali iwapo matendo ya rais yanakiuka Katiba," Farhana Khera, mkurugenzi mtendaji wa umoja wa mawakili wa Kiislam, wa shirika la kulinda haki za kiraia za Waislam wa Marekani.

Maamuzi ya rais lazima yapitiwe na mahakama

Majaji hao pia wamepinga hoja ya uongozi wa Trump kwamba mahakama hazina mamlaka ya kupitia maamuzi ya rais yanayohusu uhamiaji na usalama wa taifa.

Wamesema kwamba serikali imeshindwa kuthibitisha kwamba amri hiyo imetimiza vigezo vya kikatiba vya kutoa ilani au kuwasilisha pendekezo la amri hiyo likasikilizwa mahakamani kabla ya kupiga marufuku ya kusafiri.

Majaji hao pia wamesema uongozi wa Trump umeshindwa kuwasilisha ushahidi kwamba kuna mgeni yeyote kutoka nchi hizo saba aliyehusika na shambulio la kigaidi nchini Marekani.

Rais wa China Xi Jinping (kushoto) na Rais wa Marekani Donald Trump (kulia)Picha: Reuters/T. Melville/M. Segar

Kwa sasa, ina maana wahamiaji na raia kutoka nchi hizo saba zilizo na Waislamu wengi zilizotajwa katika amri ya rais Trump ya kushtukizia, wataendeleo kuingia nchini humo.

Wasafiri hao hawatokamatwa wakiwasili Marekani, hawatorudishwa walipotokea, na pia maandamano yanayopinga amri ya Trump na yaliyokuwa yamejaza watu ndani ya viwanja vya ndege nchini humo yatamalizika.

Trump aunga mkno sera ya "China moja"

Na kuhusu mahusiano kati ya China na Marekani, msemaji wa Ikulu ya White House amesema, Trump alifanya mazungumzo marefu na Rais wa China Xi Jinping kwa njia ya simu jana usiku, na kwamba Marekani imekubali kuheshimu sera ya China ya kile inachokiita "China moja." Kwa maana hiyo Marekani imekubali msimamo wa China kwamba kuna China moja tu na Taiwan ni sehemu yake.

Wakati huo huo, baraza la Seneti la Marekani limemuidhinisha, Tom Price, kuwa Waziri wa Afya. Kura 52 zilimuunga mkono na 47 zilimpinga.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ap/reuters

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW