Mahakama Uganda kutoa hukumu dhidi ya Thomas Kwoyelo
13 Agosti 2024Mahakama moja ya Uganda leo inatarajiwa kutoa hukumu katika kesi inayomkabili Thomas Kwoyelo, kamanda wa zamani wa kundi la wanamgambo wa Lord's Resistance Army, LRA, anayetuhumiwa kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.
Kwoyelo ambaye anakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kinyama yaliyofanywa katika mzozo wa miaka 20 kaskazini mwa Uganda, ndiye mwanajeshi wa kwanza na wa pekee wa kundi la LRA kufunguliwa mashtaka ya uhalifu wa kivita na mahakama katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Soma: ICC kutoa uamuzi rufaa ya mbabe wa kivita wa kundi la LRA
Anakabiliwa na jumla ya mashtaka 78 yakiwemo mauaji, ubakaji, kufanyisha watu utumwa, mateso na utekaji nyara miongoni mwa mashtaka mengine. Kesi hiyo inasikilizwa katika mahakama ya mji wa kaskazini mwa Uganda wa Gulu. Kwoyelo ambaye kulingana na mmoja wa mawakili wake ana umri wa miaka 49, alitekwa nyara akiwa na umri wa miaka 12. Amekanusha mashtaka yote dhidi yake.