Uingereza yahalalisha mpango wa kupelekwa wahamiaji Rwanda
20 Desemba 2022Mara tu baada ya uamuzi huo, shirika la msaada la Christian Aid imesema licha ya Rwanda kuwa katika mazingira magumu yatokanayo na athari za mabadiliko ya tabianchi, wizara ya mambo ya ndani ya Uingereza haikufanya tathmini juu ya hatari ya hali ya hewa ambayo wahamiaji hao wanaweza kukabiliana nayo ikiwa watapelekwa huko.
Chini ya makubaliano kati ya Uingereza na Rwanda yaliyofanyika mwezi Aprili, Uingereza inakusudia kuwahamisha watu wanaowasili nchini humo kinyume cha sheria kuelekea taifa hilo la Mashariki mwa Afrika, lililo kwenye umbali wa zaidi ya kilomita 6,400 kutoka Uingereza.
Shirika hilo la misaada limebaini kuwa, uamuzi huo umechukuliwa licha ya ripoti iliyotolewa mwaka huu na wizara ya mambo ya nje ya Uingereza, ambayo iliangazia vitisho lukuki vinavyohusishwa na hali ya hewa ambavyo tayari vinaiathiri Rwanda huku utabiri ukionyesha kuwa hali itakuwa mbaya zaidi katika miaka ijayo.
Soma zaidi: Uingereza yalaani uamuzi wa kuzuia waomba hifadhi kupelekwa Rwanda
Vitisho hivyo ni pamoja na uhaba wa chakula utokanao na mmomonyoko wa udongo unaosababishwa na mvua kubwa, vitisho vya kiafya vinavyohusishwa na viwango vya juu vya joto na kuongezeka kwa kuenea kwa magonjwa kama vile malaria.
Uingereza na Rwanda kuendelea na mpango wao
Kwa upande wake serikali ya Uingereza imefahamisha kuwa inaazimia kutekeleza haraka iwezekanavyo mpango huo. Msemaji wa waziri mkuu wa Uingereza, muda mfupi tu baada ya uamuzi wa Mahakama hiyo amesisitiza kuwa serikali ya London iko tayari kuutetea mpango huo wa wahamiaji dhidi ya pingamizi zote za kisheria zitakazojitokeza.
Soma zaii: Uingereza kuwapeleka Rwanda waomba hifadhi wa kwanza
Aidha, msemaji wa wizara ya Mambo ya Ndani ameutetea mpango huo na kusema ni wa kipekee na kwamba Rwanda ni nchi salama yenye rekodi ya kuwasaidia wakimbizi huku akisema dola milioni 146 zimetengwa ili kutoa msaada unaohitajika kwa wahamiaji hao ili waweze kuanzisha upya maisha yao nchini Rwanda.
Soma zaidi: Uingereza imesitisha safari ya kwanza ya waomba hifadhi kwenda Rwanda
Serikali ya Rwanda kupitia msemaji wake Yolande Makolo imeupokea vyema uamuzi wa mahakama hiyo ya juu ya Uingereza, ikisema ni hatua nzuri itakayoipa fursa ya kuchangia katika kulitafutia ufumbuzi tatizo la uhamiaji haramu duniani.
Lakini mbunge wa upinzani nchini Rwanda Frank Habineza amesema ni kosa kuwapeleka wahamiaji nchini Rwanda, taifa lenye watu wengi na lenye uhaba wa rasilimali.
Takwimu za serikali ya Uingereza zinabaini kuwa takriban wahamiaji 40,000 wamewasili nchini humo mwaka huu kwa kutumia usafiri wa mashua ndogo. Waziri Mkuu Rishi Sunak ametoa kipaumbele katika kulishughulikia suala hilo huku kukiwa na upinzani mkali kutoka kwa wanasiasa mbalimbali.