1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afisa wa kijasusi Syria ahukumiwa kifungo cha maisha jela

Sylvia Mwehozi
13 Januari 2022

Mahakama katika mji wa magharibi mwa Ujerumani wa Koblenz, imemuhukumu afisa wa zamani katika utawala wa Syria adhabu ya kifungo cha maisha jela baada ya kumkuta na hatia. 

Deutschland | Prozess um Staatsfolter in Syrien
Picha: Thomas Frey/dpa/picture alliance

Waendesha mashitaka walimtuhumu Anwar R. mwenye umri wa miaka 58 kwa mauaji aliyoyafanya kwenye gereza mjini Damascus, ambako wanaharakati wa upinzani karibu 4,000 waliteswa kati ya mwaka 2011 na 2012. Hii ni hukumu ya pili kutolewa na mahakama ya Ujerumani katika mji wa Koblenz kwa makosa dhidi ya ubinadamu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.  

Ushahidi uliowasilishwa na waendesha mashitaka ulitoa mwanga juu ya mfumo wa mateso na ukandamizaji unaofanywa na utawala wa rais wa Syria Bashar al.-Assad. Afisa huyo Anwar R anadaiwa kuwa afisa wa ngazi ya juu wa chombo cha rais Assad cha ukandamizaji na mateso. Damascus.Kesi ya kijana wa Syria mzaliwa wa Ujerumani yaanza rasmi.

Akiwa na cheo cha Kanali, Anwar R. anadaiwa kuwa mhusika wa kitengo nambari 251 cha usalama wa taifa wa Syria na jukumu la masuala ya kiusalama mjini Damascus kwa mujibu wa waendesha mashitaka wa shirikisho. Kitengo nambari 251 kilikuwa karibu na gereza. Kulingana na hati ya mashitaka, ilikuwa ni katika gereza hilo na inadaiwa chini ya uongozi wa Anwar R ambapo wafungwa wapatao 4,000 waliteswa kwa kipindi cha karibu siku 500 kati ya mwezi Aprili mwaka 2011 na Septemba 2012. 

Anwar R. raia wa Syria aliyehukumiwa kifungo cha maisha jelaPicha: THOMAS FREY/AFP

Upande wa mashitaka ulikuwa maelezo ya kina juu ya ubakaji, ”unyanyasaji mkali wa kijinsia”, unyanyasaji wa kimwili ikiwemo vichapo na kuwapiga watu shoti za umeme. Inakadiriwa kwamba wafungwa 58 walifariki gerezani kutokana na unyanyasaji huo.  Mshitakiwa wa pili Eyad A. alihukumiwa mwezi Februari mwaka jana miaka minne na nusu jela kwa makosa ya kusaidia uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Wiki moja kabla ya hukumu ya leo, timu ya mawakili wa mshitakiwa Anwar R. ilidai kuwa mteja wao alipaswa kuachiliwa huru. Wakili Yorck Fratzky alisema kuwa mshitakiwa hakuwahi kutenda makosa ya utesaji wala kutoa maelekezo ya kufanya hivyo. Aliongeza kuwa afisa huyo aliwahi kupanga kwa ajili ya wafungwa kuachiwa huru. 

Uwezo wa waendesha mashitaka wa Ujerumani wa kusikiliza kesi dhidi ya raia wa Syria wanaotuhumiwa kwa mateso na mauaji ya Wasyria wengine katika mahakama za Ujerumani, unaongozwa na kanuni ya uhalifu dhidi ya sheria ya kimataifa iliyoanza kutumika Juni mwaka 2002. 

Kanuni hiyo inajumuisha kile kinachojulikana kama misingi ya mamlaka ya ulimwengu inayoruhusu mahakama za Ujerumani kushitaki uhalifu dhidi ya sheria ya kimataifa hata kama uhalifu huo haukufanywa ndani ya Ujerumani na mshitakiwa si raia wa Ujerumani. Mashahidi wengi waliingia Ulaya kama wakimbizi na baadhi yao walipata makaazi Ujerumani. Wanawake na wanaume 17 waliotoa ushahidi wao wanaungwa mkono na kituo cha Ulaya cha haki za kikatiba na kibinadamu (ECCHR). Tisa kati yao ni walalamikaji wa pamoja katika kesi dhidi ya Anwar R.  

Mamlaka za Ujerumani zimekuwa zikifanya uchunguzi dhidi ya uhalifu wa utawala wa Assad tangu mwaka 2011. Waendesha mashitaka wanapokusanya ushahidi wa kutosha dhidi ya mshitakiwa fulani, huanzisha uchunguzi wa awali dhidi yake. Kiasi ya maafisa 20 waandamizi wa Syria wamefunguliwa mashitaka.  

Mwanamke wa Syria akiwa amebeba picha za jamaa zake waliouwawa Picha: Martin Meissner/AP Photo/picture alliance

Ushahidi huo unakusanywa na "kitengo cha uhalifu wa kivita" katika ofisi ya shirikisho la uhalifu la Ujerumani. Wachunguzi walipata usaidizi muhimu kutoka taasisi yenye makao yake makuu nchini Uholanzi: Tume ya haki ya kimataifa na uwajibikaji (CIJA), ambayo ilisafirisha maelfu ya nyaraka za serikali kutoka Syria baada ya vita kuanza. 

Anwar R. aliingia Ujerumani mnamo mwaka 2014 na familia yake, kisha akaomba hifadhi na kupewa ukaazi mjini Berlin. Akiwa na hofu ya kwamba alikuwa akifuatiliwa na usalama wa taifa wa Syria, aliwasiliana na polis iwa Ujerumani. Walimhoji na afisa huyo aliwajibu kuhusu muda alichokuwa akifanya nchini Syria. Vyanzo vilivyo karibu na uchunguzi huo viliiambia DW kwamba Anwar R. bila shaka hakufikiria kuwa angeshtakiwa.

Wanasema alisimulia hadithi yake bila hisia yoyote dhahiri ya kufanya makosa. Baada ya miezi kadhaa ya uchunguzi wa ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa shirikisho, Anwar R. alikamatwa mnamo Februari 12, 2019. 

Hukumu ya leo pia inaweza kutoa uelewa bora wa jumla wa utawala dhalimu wa Syria, ambao unaweza kutumika kama kielelezo cha kesi nyingine nchini Ujerumani au kwingineko. Msemaji wa Ofisi ya mwendesha mashtaka wa shirikisho aliiambia DW kwamba ushahidi wanaokusanya unaweza kutumika kwa miongo kadhaa ijayo.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW