1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya Ulaya yaruhusu marufuku ya hijabu kazini

14 Machi 2017

Mahakama ya Haki ya Ulaya, ECJ imesema waajiri binafsi wanaweza kuwapiga marufuku wafanyakazi wa kike kuvaa vazi linalofunika kichwa, hijab.

MUSLIMS IN AMERICA: Hannah Shraim,
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Martin

Mahakama ya ECJ imesema katika uamuzi wake ulitolewa Jumanne(14.03.207) kuhusu kesi mbili zinazomuhusisha mhandisi wa programu ya kompyuta nchini Ufaransa ambaye alikuwa akivaa hijab pamoja na karani wa mapokezi nchini Ubelgiji ambaye pia alikuwa akivalia vazi hilo maarufu ambalo huvaliwa na wanawake wa Kiislamu.

Uamuzi huo mgumu umetolewa katika kesi iliyofunguliwa mwaka 2003 wakati Samira Achbita, mwanamke wa Kiislamu aliyeajiriwa kama karani wa mapokezi kwenye kampuni ya huduma za usalama ya G4S nchini Ubelgiji.

Mahakama ya ECJ imesema wakati huo, kampuni hiyo haikuwa na sheria yoyote ya maandishi inayosema kwamba wafanyakazi wake hawaruhusiwi kuvaa kazini aina yoyote ya mavazi yenye utambulisho wa kisiasa, kidini au falsafa.

Mwaka 2006, Achbita aliiambia G4S kwamba anataka kuvaa hijab kazini, lakini akaambiwa haruhusiwi. Baada ya hapo kampuni hiyo ilitangaza rasmi kupiga marufuku mavazi ya aina hiyo. Achbita alifukuzwa kazi hatua iliyosababisha aende mahakamani kufungua kesi ya ubaguzi.

Mwanamke wa kiislamu Samantha Elauf nchini MarekaniPicha: Reuters/J. Bourg

Katika uamuzi huo juu ya suala ambalo limekuwa la kisiasa barani Ulaya, Mahakama ya ECJ imesema uamuzi wa kupiga marufuku mavazi ya aina hiyo haukuwa na ubaguzi wowote kwa kuzingatia misingi ya kidini, wala haukwenda kinyume cha sheria, ikiwa vigezo vingine kadhaa vilizingatiwa.

Uamuzi huo uliotolewa na mahakama ya ECJ iliyoko Luxembourg, umetolewa siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi wa wabunge nchini Uholanzi, ambao suala la uhamiaji na uislamu limekuwa likizungumziwa kwa kiasi kikubwa.

Mawakili katika mahakama hiyo ya juu barani Ulaya, wametoa maoni yanayokinzana jinsi ya kutafsiri maelekezo na hukumu za awali zilizotolewa na mahakama za rufaa za Ufaransa na Ubelgiji.

Wakili mkuu, Eleonor Sharpston amesema kuhusu kesi ya mfanyakazi wa Ufaransa mhandisi wa programu ya kompyuta, Asma Bougnaoui ambaye alifukuzwa kazi mwaka 2009 kwa kuvaa hijab wakati akimpatia ushauri mteja wa Toulouse, huenda ilikiuka sheria ya Umoja wa Ulaya inayozuia ubaguzi kwa misingi ya kidini. ECJ imesema haki kwa kila mfanyakazi kudhihirisha dini yake, inapaswa kutolewa.

Ili kuhakikisha wananchi ndani ya Umoja wa Ulaya wanashiriki kikamilifu, ikiwemo maisha ya kiuchumi, Mwongozo namba 200/78 wa Umoja wa Ulaya unakataza ubaguzi wowote ule, uwe wa moja kwa moja au usio wa moja kwa moja. Maelekezo hayo yanatokana na Mkataba wa Umoja wa Ulaya kuhusu Haki za Msingi uliopitishwa mwaka 2000 pamoja na mkataba mwingine wa zamani wa Roma kuhusu Haki za Msingi na Uhuru, ambao uliofikiwa mwaka 1950.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, DPA, Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW