Mahakama ya Ulaya yatoa hukumu kesi ya ushindani ya Meta
5 Julai 2023Mahakama ya Haki ya Umoja wa Ulaya imetoa uamuzi kuwa mataifa wanachama wana haki ya kusimamia uzingatiaji wa siri za watumiaji wa kampuni za teknolojia. Mahakama hiyo ya ECJ imesema mamlaka za mataifa wanachama zinazohusika na masuala ya ushindani wa kibiashara zinapaswa kuangalia kama kampuni zinazingatia sheria za ulinzi wa data. Uamuzi wa mahakama hiyo unafuatia shirika la ushindani la Ujerumani kuiamuru Meta ambayo ni kampuni mama ya mitandao ya kijamii ya Facebook, Whatsapp na Instagram kuwacha kukusanya data za watumiaji bila idhini yao. Haya yalijiri wakati shirika hilo lilisema Facebook iliwalazimu watumiaji kuafiki kuhusu ukusanyaji wa data wakati wanapofungua akaunti zao. Shirika hilo lilihoji kuwa kifungu hicho hakikumaanisha idhini ya hiari kutokana na jukumu kuu la soko la mtandao huo wa kijamii. Kampuni ya Meta ilikuwa imepinga suala hilo, ikihoji kuwa shirika hilo la Ujerumani lilikiuka mamlaka yake. Shirika hilo kisha likatafuta ushauri wa mahakama ya ECJ.