Mahakama ya UN yaipa ushindi Qatar kesi ya kufungiwa anga
15 Julai 2020Mahakama ya Haki ya Kimataifa, ICJ, imekataa rufaa ya Bahrain, Misri, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu kupinga uamuzi wa Juni 2018 wa shirika la kimataifa la usafiri wa anga, ICAO na kutupilia mbali upinzani wa mataifa hayo dhidi ya mamlaka ya shirika hilo kuamua mzozo huo wa usafiri anga.
Hukmu hiyo inalisafishia njia shirika la ICAO kuweza kuamua katika shauri la Qatar lililowasilishwa Oktoba 2017, ikidai kwamba ususiaji dhidi yake ulikiuka mkataba wa kimataifa unaosimamia usafrii wa kimataifa. Waziri wa usafirishaji na mawasiliano wa Qatar, Jassim Saif Ahmed Al-Sulaiti ameikaribisha hukumu.
"Tuna imani kwamba hatimaye ICAO itayabaini matendo hayo kuwa kinyume cha sheria," alisema. "Hii ndiyo hukumu ya karibuni katika mkururu wa hukumu zinazodhirisha upuuzaji wa sheria na taratibu za kimataifa unaofanywa na mataifa yalioiwekea mzingiro Qatar. Hoja zao zinavunjwa hatua kwa hatua, na msimamo wa Qatar umethibitishwa."
UAE kutoa maelezo kwa ICAO
Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu nchini Uholani, Hissa Abdullah Al Otaiba, alisema uamuzi huo ulikuwa wa "kiufundi na unahusu tu masuala ya taratibu na mamlaka ya kushughulikia mgogoro; Haukuzingatia uhalali wa kesi." Alisema Umoja wa Falme za Kiarabu utatoa maelezo kwa ICAO kwa nini uliweka vikwazo dhidi ya ndege za Qatar.
Rais wa mahakama hiyo ya ICJ, yenye makao yake mjini The Hague Abdulqawi Ahmed Yusuf alisema mahakama hiyo kwa kauli moja iliipinga rufaa hiyo iliyowasilishwa na mataifa hayo dhidi ya Qatar, yakipinga uamuzi wa ICAO, ulioipendelea Qatar, kuhusiana na uhuru wa kutumia anga zao.
Misri, Bahrain, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu walikata mahusiano ya kidiplomasia na Qatar msimu wa joto wa mwaka 2017, kwa madai kwamba inayafadhili makundi ya upinzani ya Kiislamu ambayo mataifa hayo yanayachukulia kama makundi ya kigaidi.
Aidha, mataifa hayo pia yalikata mahusiano ya kiuchumi na Qatar, kuzuia ndege za Qatar kupita kwenye maeneo yao ya anga, kufunga mipaka na kuzuia meli za Qatar kutumia bandari zao.
Chanzo: AFP/AP