1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroKimataifa

Mahakama UN yaitaka Israel kuepusha mauaji ya kimbari Gaza

26 Januari 2024

Mahakama ya Umoja wa Mataifa ICJ imeiamuru Israel kuzuwia vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina, na kuchukua hatua za kuwasaidia raia, ingawa imesita kuamuru usitishaji mapigano kama ilivyota Afrika Kusini.

The Hague, Uholanzi | Mahakama ya Haki ya Kimataifa| Kesi ya mauaji ya kimbari dhidi ya Israel | Utoaji wa hukumu
Mahakama ya ICJ imeitaka Israel kuepusha mauaji ya kimbari Gaza, lakini imesita kuitaka isitishe vita dhidi ya Hamas.Picha: Remko de Waal/ANP/AFP/Getty Images

Mahakama hiyo ya juu ya kimataifa imesema Israel laazima ihakikishe vikosi vyake havitekelezi vitendo vya mauaji ya kimbari na kuitaka ichukuwe hatua kuboresha hali ya kiutu kwa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Hata hivyo haikutoa uamuzi kuhusu kiini cha kesi hiyo iliyofunguliwa na Afika Kusini - cha iwapo mauaji ya kimbari yametendeka Gaza. Lakini imetambua haki ya Wapalestina wa Gaza kulindwa dhidi ya vitendo vya mauaji ya kimbari.

Katika hukumu yao, majaji 15 kati ya 17 wa ICJ wamepigia kura hatua za dharura zilizoshughulikia sehemu kubwa ya mambo ambayo Afrika Kusini iliyaomba, isipokuwa suala la kuamuru usitishaji wa hatua za kijeshi za Israel Gaza, ambazo zimesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 25,000 kulingana na wizara ya Ukanda huo inayosimamiwa na Hamas.

''Taifa la Israel litachukuwa hatua zote zilizoko ndani ya mamlaka yake kuzuwia na kuadhibu uchochezi wa moja kwa moja na wa wazi wa mauaji ya kimbari, kuhusiana na wanachama wa kundi la Wapalestina katika Ukanda wa Gaza'', alisema Rais wa ICJ Joan Dongoghue wakati akisoma uamuzi wa majaji.

Watu wanaoiunga mkono Palestina wakishangilia baada y ahukumu ya mahakama ya Umoja wa Mataifa, ICJ, kuhusu hatua za dharura dhidi ya Israel, kufuatia tuhuma za Afrika Kusini kwamba operesheni ya kijeshi ya Israel ni mauaji ya kimbari yanayofanywa na serikali.Picha: Alet Pretorius/REUTERS

Mahakama imesema ina wasiwasi mkubwa kuhusu hatma ya mateka wa Israel wanaoshikiliwa Gaza, na kuitaka Hamas na makundi mengine kuwaachia mara moja mateka hao bila masharti.

Soma piaIsrael yazidi kushinikizwa kusitisha mapigano Gaza

Lakini hukumu hiyo ambayo imekaribishwa na Wapalestina, bado itakuwa fedheha kwa Israel na washirika wake wa karibu, ikiwemo Marekani na Ujerumani.

Israel inatakiwa kuripoti mahakamani hapo juu ya hatua inazozichukua kutekeleza maagizo yake katika muda wa mwezi mmoja. Lakini wakati maamuzi ya ICJ ni ya mwisho na hayana rufaa, mahakama hiyo haina njia ya kulazimisha utekelezaji wake.

Ushindi wa utawala wa sheria wa kimataifa

Afrika Kusini imesifu uamuzi huo wa ICJ na kuutaja kuwa ushindi mkubwa wa utawala wa sheria wa kimataifa na hatua kubwa katika kutafuta haki kwa watu wa Palestina, imesema wizara ya mambo ya nje ya taifa hilo.

Watu wakishika na kuepeperusha bendera wakati wa maandamano ya Wapalestina nje ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) huku majaji wakitoa uamuzi kuhusu hatua za dharura dhidi ya Israel kufuatia shutuma za Afrika Kusini kwamba operesheni ya kijeshi ya Israel Gaza ni mauaji ya kimbari yanayoongozwa na serikali, mjini The Hague, Uholanzi, Januari 26, 2024.Picha: Piroschka van de Wouw/REUTERS

Rais Cyrill Ramaphosa na kamati ya chama tawala cha ANC, walikatisha mkutano wao na kuanza kushangilia uamuzi wa ICJ.

Palestina imekaribisha hukumu hiyo huku waziri wake wa mambo ya nje Riyad al-Maliki, akiyatolea wito mataifa kuhakikisha hatua zilizoamriwa na mahakama zinatekelezwa.

Ujerumani ambayo ni mshirika wa karibu wa Israel imesema itaheshimu uamuzi wa mahakama, huku Uhispania, Uturuki na mataifa mengine pia yakielezea kuridhishwa na uamuzi huo.

Hata hivyo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, amekosoa uamuzi huo, na kusisitiza kuwa mashtaka ya Afrika Kusini siyo tu ya uongo, bali pia ni ya kukasirisha, na kwamba watu wote wenye heshima duniani wanapaswa kuyakataa.

Netanyahu amesema utayari wa ICJ kujadili madai ya mauaji ya kimbari dhidi ya Israek ni aibu ambayo haitafutika kwa vizazi kadhaa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW