Mahakama ya upatanishi kuamua rufaa za wanariadha wa Urusi
22 Januari 2018Mahakama ya upatanishi katika michezo imeanza wiki nzima ya kusikiliza rufaa kwa wanariadha 39 wa Urusi ambao wamefutiwa ushindi wao katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 2014 mjini Sochi , Urusi kwa kushiriki katika mpango wa taifa hilo wa kutumia madawa ya kuongeza nguvu misuli , yaani doping.
Mahakama hiyo ya CAS inatarajia kutoa hukumu wiki ijayo. Baadhi ya wanariadha wanamatumaini ya kubadilisha hukumu za kutoshiriki mashindano ya olimpiki maisha na kushiriki katika michezo ya olimpiki ya majira ya baridi mjini Pyeongchang nchini Korea kusini.
Mashahidi wawili muhimu, mtu aliyefichua njama za Urusi za kutumia madawa hayo Grigory Rodchenkov na mchunguzi wa shirika la kupambana na madawa hayo duniani Richard McLaren , wanatarajiwa kutoa ushahidi kwa njia ya vidio ama kwa simu katika kusikilizwa kwa kesi hizo ambako kunafanyika kwa faragha katika kituo cha mikutano mjini Geneva.
Na rais wa FIFA Gianni Infantino na mwenzake wa shirika la vyama vya riadha duniani IAAF Sebastian Coe huenda wasiwekwe katika uanachama wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki mwezi ujao licha ya kusubiri kwa miaka mitatu, duru zimesema hii leo.
Mashirika hayo mawili ya kimataifa , miongoni mwa michezo maarufu katika olimpiki , yamepuuzwa tangu mwaka 2015 wakati wakihangaika kupambana na rushwa iliyotanda katika mashirika yao pamoja na kashfa za rushwa ambazo zimechafua heba yao.
IOC inachagua wanachama wapya katika kikao cha kila mwaka ambapo orodha ya majina yaliyopendekezwa yanachapishwa siku chache kabla ya kupigiwa kura.
Mwandishi : Sekione Kitojo / ape / rtre / dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga