Mahakama yamthibitisha Kabila kuwa mshindi
17 Desemba 2011Akisoma uamuzi wa Mahakama hiyo, Jaji Jerome Kitoko alisema kuwa upande wa Kamerhe haukuwasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha hoja yao.
Hatua hiyo ya jana (16.12.2011) jioni ya mahakama hiyo, imeongeza hali ya wasiwasi wa vurugu zaidi katika taifa hilo kubwa kabisa kusini mwa jangwa la Sahara, kwani tayari mgombea wa chama kikuu cha upinzani, Etienne Tshisekedi, ameshayakataa matokeo yaliyomuweka yeye nafasi ya pili.
Uchaguzi wa Novemba 28 ulikuwa ni wa pili tu wa kidemokrasia katika historia ya miaka 51 ya uhuru wa nchi hiyo, na wa kwanza kuratibiwa na serikali ya Kongo bila ya ushiriki wa jumuiya ya kimataifa.
Waangalizi wa uchaguzi huo wameeleza wasiwasi wao wa kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi, wakisema kuwa katika baadi ya wilaya idadi ya waliojitokeza kupiga kura ilikuwa kubwa mno kiasi ya "kutowezekana."
Rais wa sasa, Joseph Kabila, alikuwa akikabiliana na wagombea 10 akiwemo Tshisekedi, mzee wa miaka 79 mwenye umaarufu sana katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa rasilimali lakini lenye "umasikini wa kutupwa".
Waangalizi wanahofia kutokea machafuko ikiwa Tshisekedi atawaamuru wafuasi wake kuandamana. Hadi sasa, Tshisekedi amewataka wafuasi wake kutulia kusubiri maagizo yake.
Kwa mara ya kwanza, Kabila aliingia madarakani baada ya kuuawa kwa baba yake, Laurent Kabila, miaka kumi iliyopita. Matokeo yaliyotolewa wiki iliyopita yalionesha kuwa alipata asilimia 49 ya kura, huku Tshisekedi akiwa na asilimia 32 katika karibuni kura milioni 19 zilizopigwa.
Hata hivyo, siku moja tu baada ya matokeo hayo kutangazwa, waangalizi wa Marekani kutoka kituo cha Carter, kilichoasisiwa na rais wa zamani wa nchi hiyo, Jimmy Carter, kilitoa taarifa inayosema kuwa uchaguzi huo ulikosa uhalali.
Mmoja wa waangalizi wakuu wa kituo hicho, David Pottie, alisema kwamba kwamba ni "jambo lisilowezekana kuwa na asilimia 100 ya wapiga kura katika maeneo ambayo chini ya asilimia 2 ya barabara zimetengenezwa, ambako pia kura zote zimekwenda kwa Kabila, huku kukiwa na wagombea 11 kwenye karatasi ya kura".
Hapo kabla, wataalamu wa masuala ya Kongo na wapinzani waliitaka serikali kuzuia upigaji kura kutokana na matatizo kadhaa ya kiufundi. Hata hivyo, upigaji kura uliendelea na kazi ya kuhisabu kura ilisogezwa mbele kwa siku kadhaa.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, iliyo katikati ya bara la Afrika, ni taifa kubwa sana, likiwa sawa na Ulaya Magharibi nzima na ikipakana na mataifa mengine tisa. Baadhi ya wilaya za nchi hiyo, ambayo ilikandamizwa kwa miaka kadhaa ya udikteta na vita viwili vya wenyewe kwa wenyewe, ziko mbali sana kiasi ya kwamba masanduku ya kura yalipaswa kusafirishwa kupitia barabara za matope juu ya vichwa vya wapagazi na pia kupitia mitumbwi kwenye mito.
Uchaguzi wa mwaka huu ulifanyika huku kukiwepo machafuko katika maeneo ya mashariki ya Kongo, ambako makundi kadhaa ya waasi wameendelea kutishia usalama wa watu na mali zao. Wanajeshi wa serikali na waasi wanashutumiwa kwa kuwabaka wanawake, wanaume na watoto, na kuvichoma moto vijiji. Mamia kwa maelfu ya watu wamelazimika kuyakimbia makaazi yao kutokana na vurugu hizo.
Mapigano yanachochewa na ushindani wa kumiliki migodi, ambayo mingi yao inaendeshwa na wanajeshi na waasi, ambao hutumia mapato ya madini kuimarisha makundi yao yenye silaha.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Sudi Mnette