1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama yamuondolea Morsi adhabu ya kifo

22 Novemba 2016

Mahakama hiyo ya mjini Cairo imeamuru kesi hiyo kusikilizwa upya. Hii ni mara ya pili Morsi anashinda kesi ya rufaa. Wiki iliyopita mahakama hiyohiyo ilibatilisha hukumu nyingine ya kifo dhidi yake.

Ägypten Mohamed Morsi Ex-Präsident im Gerichtssaal
Picha: Imago/ZUMA Press

Mahakama ya juu kabisa nchini Misri imefutilia mbali adhabu moja ya kifungo cha maisha aliyopewa rais aliyepinduliwa madarakani Mohammed Morsi. Mahakama hiyo imeamuru kesi hiyo kusikilizwa upya.

Uamuzi wa mahakama hiyo ya mjini Cairo unajiri takriban miezi 17 baada ya hukumu ya awali dhidi ya Morsi, ambaye anatokea vuguvugu ambalo sasa limepigwa marufuku la Udugu wa Kiislamu yaani Muslim Brotherhood. Mohammed Morsi alishtakiwa kwa makosa ya kushirikiana na makundi ya kivita ya kigeni likiwemo kundi la Hamas kutoka Palestina  ambalo linasimamia ukanda wa Gaza.

Hii ni mara ya pili Morsi anashinda kesi ya rufaa. Wiki iliyopita mahakama hiyohiyo ilibatilisha hukumu ya kifo dhidi yake katika kesi tofauti iliyohusiana na jaribio la kutoroka gerezani wakati wa mapinduzi ya mwaka 2011 dhidi ya aliyekuwa mtangulizi wake Hosni Mubarak. Kesi ambayo Morsi alipewa adhabu ya kifo.

Kando na Morsi, korti hiyo pia ilifutilia mbali hukumu za kifungo cha maisha jela kwa wafungwa wengine 16 ambao ni wanachama wa vuguvugu la Udugu wa Kiislamu, akiwemo kiongozi wa kidini wa kundi hilo  Mohammed Badei. Katika uamuzi wao, majaji walisema: "Korti imeamua kwanza kukubali pingamizi la muendesha mashtaka kuhusu kesi. Pili korti imekubali rufaa ya mhukumiwa na kesi kurudiwa."

Mkuu wa vuguvugu la Udugu wa Kiislamu Mohammed BadiePicha: picture alliance/dpa/M. A. Ghani/A. Al

Aidha mahakama ilibatilisha adhabu ya kifo kwa kiongozi mashuhuri wa kundi hilo Khairyat el-Shater na wengine 15. Hakuna tarehe kamili iliyotangazwa ya kusikilizwa kwa kesi hizo.

Mwezi uliopita  mahakama ilikataa kubatilisha adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela kwa Morsi, kufuatia mashtaka ya kuwaua waandamanaji mnamo Disemba mwaka 2012. Hiyo ilikuwa hukumu ya kwanza dhidi ya Morsi ambaye utawala wake ulizua mgawanyiko kabla ya kupinduliwa na jeshi mwaka 2013, mwaka mmoja tu tangu alipochukua urais.

Tangu kupinduliwa kwake Morsi amekuwa kivyake huku akikumbwa na mashtaka kadhaa.

Uamuzi wa mahakama unajiri wakati maafisa nchini Misri wamelitaja vuguvugu la udugu wa Kiislamu kuwa la kigaidi na wanaendelea kuliandama ikiwa ni pamoja na  wanachama na wafadhili wake kando na kulipiga marufuku. Mnamo Jumatatu, kamati inayohusika na masuala ya  sheria  iliamuru mali za wanachama 45 wa kundi hilo kutwaliwa.

Mwandishi: John Juma/ AFPE/DPE

Mhariri: Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW