Mahakama yasitisha marufuku ya mikutano ya kisiasa Kenya
19 Agosti 2021Kwa mujibu wa Jaji Anthony Mrima, kamati ya usalama wa taifa haina mamlaka ya kuiamuru idara ya polisi kutawanya mihadhara au mikutano yoyote kwani inajisimamia katika wizara ya usalama wa taifa. Mahakama kuu pia imemuamuru Inspekta mkuu wa polisi Hilary Mutyambai kutoshinikiza utekelezaji wa agizo la serikali la kutawanya na kutoa ridhaa ya mihadhara ya kisiasa kufanyika.
Itakumbukwa kuwa tarehe 7 mwezi wa Oktoba kamati ya usalama wa taifa ilitangaza marufuku ya mikutano na mihadhara ili kutuliza hali baada ya mahasimu wa kisiasa waliokuwa kwenye shughuli kanisani huko Muranga kupapuana.
Naibu wa rais William Ruto alihudhuria kikao hicho kilichozua maafa baada ya vurugu kutokea. Kauli ya mahakama inajiri saa chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza jana jioni kuwa muda wa kutotoka nje usiku umeongezwa kwa siku 60 zijazo.
Rais Uhuru aliyasema hayo baada ya kufanya kikao kwenye ikulu ya Mombasa na viongozi wa siasa wa upinzani pamoja na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe.
''Vizuwizi ni maandalizi ya matukio ya kijacho''
Hata hivyo, chama cha mawakili nchini Kenya,LSK, kiliwasilisha kesi mahakamani na kutaka marufuku ya kutotoka nje usiku kufutiliwa mbali kadhalika mihadhara kwa madai kwamba inawalenga baadhi ya viongozi wa siasa.Nelson Havi ni mwenyekiti wa chama cha mawakili nchini Kenya.
'' Kuna wasiwasi kuwa marufuku ya kutotoka nje usiku ni maandalizi ya matukio ya kijacho wakati wa uchaguzi ili ukiukwaji wa katiba na sheria uendelee. Vizuwizi lazima viondolewe.'',alisema Havi.
Viongozi wa kisiasa wana mtazamo huohuo kama anavyosisitiza Maina Kamanda, mbunge wa zamani wa Starehe.
''Wanaofaidika na hatua hii ya vizuwizi ni polisi pekee'',alisema.
Ni wachache waliopewa chanjo
Yote hayo yakiendelea, idara ya afya katika kaunti ya Nairobi imeweka bayana kuwa 10% ya wakaazi wake wamepata chanjo ya covid 19 mpaka sasa. Shughuli ya kutoa chanjo ilizinduliwa miezi sita iliyopita.
Kulingana na waziri wa afya katika kaunti ya Nairobi Dr Ouma Oluga,chanjo inatakikana kwa wingi kwani umma haujasuasua.Kwa sasa Kenya inasubiri kupokea chanjo za Johnson and Johnson na Modena zinazotarajiwa kuwasili wiki ijayo.