Mahakama yathibitisha ushindi wa Azali Assoumani
3 Aprili 2019Matangazo
Azali alitangazwa mshindi kwa kupata asilimia 59 ya kura dhidi ya mpinzani wake Mohammoudou Ahamada aliyenyakua asilimia 15.7 ya kura na Mouigni Baraka Said Souilihi alichukua nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 5.5 ya kura.
Jaji wa mahakama ya juu Harmia Ahmed akitangaza uamuzi wa mahakama hiyo alisema kutokana na Azali Asoumani kupata wingi mkubwa wa kura anatangazwa rais wa jamhuri ya visiwa vya Comoro.
Matokeo hayo yaliidhinishwa katika mahakama kukiwa na usalama wa hali ya juu mjini Moroni.
Upinzani umelalamika kwamba kulikuweko na wizi mkubwa wa kura na dosari chungunzima katika uchaguzi uliofanyika Machi 24.
Waangalizi na mashirika ya kijamii yamehoji uhalali wa uchaguzi huo.