1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maharamia wa Somalia waiteka Meli ya Mafuta katika pwani ya nchi hiyo.

Eric Kalume Ponda18 Novemba 2008

Kwa mara nyingine maharamia wanaoendesha shughuli zao katika pwani ya Somalia wameiteka Meli inayosafirisha mafuta katika eneo hilo la upembe mwa Africa.

Maharamia waiteka meli ikiwa na shehena kubwa zaidi kuwahi kutekwa na maharamia katika pwani ya Somalia.Picha: AP


Kwa mara nyingine maharamia wanaoendesha shughuli zao katika pwani ya Somalia wameiteka Meli inayosafirisha mafuta katika eneo hilo la upembe mwa Africa.


Meli hiyo ya Saudi Arabia imetekwa nyara ikiwa na shehena ya mafuta ambayo hayajasafishwa,na kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa hii ndio meli kubwa zaidi kuwahi kutekwa nyara na maharamia hao katika Pwani hiyo ya Somalia

Meli hiyo MV Sirius mali ya kampuni kubwa ya mafuta ya Aramco nchini Saudi, imetekwa nyara ikiwa na jumla ya mapipa milioni 2 ya mafuta ambayo hayajasafishwa ya thamani ya dola millioni 100, hii ikiwa shehena kubwa zaidi kuwahi kutekwa nyara na maharamia hao katika siku za hivi punde.

Kulingana na afisa wa jeshi la Marekani linaloshika doria katika pwani hiyo ya Somalia Micheal Mullen, meli hiyo ilitekwa nyara ikiwa na jumla ya wafanyi kazi 25, raia wa Croatia, Ufilipino, Uingereza,Saudia ambao wote wako salama.


Meli hiyo ilitekwa nyara katika pwani ya Somalia, yapata umbali wa kilomita 450 kaskazini masharimki mwa mji wa bandari wa Mombasa nchini Kenya.


Kisa hiki kimetokea siku chache tu baada ya jumuiya ya Ulaya kuanzisha doria ya pamoja ya usalama wiki iliyopita katika pwani hiyo ya somalia, ambayo inatajwa kuwa hatari zaidi kwa vyombo vya usafiri wa baharini.


Kulingana na msemaji wa jeshi la Marekani katika eneo la Bahrain Jane Campell, meli hiyo bado inazuiliwa na maharamia hao na hadi sasa hakuna juhudi zozote zilizofanikiwa kuikomboa meli hiyo.


Kisa hiki kimetoka miezi michache tu baada ya maharamia hao kuiteka meli nyingine iliyokuwa na shehena ya silaha zilizodaiwa kusafirishwa hadi Kusini mwa Sudan, ingawa madai hayo yalipingwa vikali na serrikali ya Kenya,ikisema kuwa shehena hiyo ni yake.


Shirika la kimataifa la usafiri wa vyombo vya baharini linasema kuwa jumla ya meli 83 zimeshambuliwa katika pwani hiyo ya Somalia,huku meli 33 zikitekwa nyara tangu mwezi Januari mwaka huu.

Kati ya hizo, jumla ya meli 12 zikiwa na jumla ya wafanyi kazi 200, bado zinazuiliwa na maharamia hao.katika pwani hiyo ya Somalia.


Hatua hii imetoka huku hali ya usalama nchini humo ikizidi kuzorota kufuatia mashambulizi ya wapiganaji wa Kislamu wanaoipinga serikali ya Rais Abdullahi Yusuf.


Wapiganaji hao tayari wameiteka miji kadhaa na sasa wanadaiwa kuukaribia mji mkuu wa Mogadishi.


Rais Yusuf alikiri hivi majuzi mji mkuu wa Nairobi nchini Kenya, kwamba imekuwa vigumu kudumisha usalama nchini mwake ambako eneo kubwa sasa linasimamiwa na wapiganaji hao wa kiislamu.


Somalia haijakuwa na serikali dhabiti kwa zaidi ya muda wa miaka 17, tangu kutimuliwa madarakani kwa aliyekuwa dikteta Siad Barre, hali inayozidisha visa vya uharamia katika pwani ya nchi hiyo.



Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW