1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahasimu wa kisiasa wa Sudan Kusini wakutana Kahrtoum

26 Juni 2018

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amesema anatarajia mkutano wake na hasimu wake mkubwa Riek Machar utaleta mafaniko ya kuvimaliza vita nchini mwao

Südsudan Riek Machar  Salva Kiir
Picha: picture-alliance/AP/J. Patinkin

Rais Salva Kiir na hasimu wake Riek Machar walikutana kwenye kituo cha mikutano cha mjini Khartoum kwa mazungumzo mapya baada ya mkutano wao uliofanyika wiki iliyopita nchini Ethiopia kushindwa kufikia mafanikio yoyote.

Machar pia amesema ana matumaini kuwa amani inaweza kupatikana Sudan Kusini, ambako maelfu ya watu wameuawa na karibu watu milioni nne wamelazimika kuyahama makazi yao tangu mapigano yalipoanza Desemba 2013.

Mipango ya hivi karibuni ya mazungumzo kati ya mahasimu hao wakubwa imefanyika baada ya viongozi wa Afrika Mashariki kuanzisha jitihada mpya za kutafuta amani nchini Sudan Kusini, ambako vikundi vya wapiganaji vinakabiliwa na tarehe ya mwisho ili kuzuia vikwazo vya Umoja wa Mataifa.

Mazungumzo ya kwanza yaliyovunjika yalifanyika siku ya Alhamisi iliyopita mjini Addis Ababa yaliandaliwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na mkutano wa jana Jumatatu wa huko Khartoum uliandaliwa na Rais wa Sudan Omar al-Bashir na kuhudhuriwa na Rais wa Uganda Yoweri Museveni.

Rais wa Sudan Omar Al BashirPicha: Reuters/M. Abdallah

Ahmed Soliman, ni mtafiti mwandamizi katika kitengo cha Afrika cha shirika la Chatham House jijini London, Uingereza. Anazungumzia jukumu na rais wa Sudan Omar Hassan al Bashir katika kuyasimamia mazungumzo kati ya rais Kiir na Machar, na kwa nini anaamini yanaweza kufaulu kuwapatanisha mahasimu hao wawili akisaidiwa na rais wa Uganda, Yoweri Museveni.

Soliman amesema bila shaka rais Bashir na rais Museveni watawashinikiza zaidi viongozi hao wawili, hasa katika kujadili na kukubaliana juu ya masuala yenye utata yaliyopo. Museveni na Bashir wote ni wadau wenye ushawishi mkubwa nchini Sudan Kusini na katika kanda hiyo, na bila shaka wana uwezo wa kupunguza tofauti kubwa zilizopo kati ya viongozi wa Sudan Kusini.

Rais wa Uganda Yoweri MuseveniPicha: Reuters/J. Akena

Haijulikani ni kwa muda gani viongozi hao wawili watakuwepo mjini Khartoum, lakini wajumbe wao wamepangiwa kuzungumza kwa wiki mbili zijazo juu ya masuala mazito ikiwa ni pamoja na mipango ya kugawana madaraka na usalama wa Sudan Kusini. Baadae Wajumbe wa pande zote mbili watasafiri kwenda Nairobi kwa mazungumzo zaidi.

Mnamo mwezi Mei, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa muda wa mwezi mmoja ili pande hizo mbili kufikia mkataba wa amani au sivyo zitawekewa vikwazo.

Rais al Bashir amesema mgogoro wa Sudan Kusini umeathiri usalama wa kanda nzima ndio maana jumuiya ya kimataifa inafikiria kuziwekea vikwazo pande hizo mbili. Hata hivyo rais Bashir amesema Sudan haiwezi kuiwekea vikwazo Sudan ya Kusini kwa sababu vikwazo hivyo vitawaongezea mateso raia wa Sudan Kusini.

Mwandishi:Zainab Aziz/AFPE

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

 

 

 

 

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW