1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahasimu wa Libya wakubaliana kuandaa uchaguzi Desemba 10

29 Mei 2018

Pande zinazohasimiana Libya zimekubaliana katika tamko litakalotoa suluhu ya kisiasa nchini mwao, kufanya uchaguzi utakaosimamiwa na Umoja wa Mataifa mwezi Desemba ili kumaliza mgogoro wa miaka saba.

Libyen UN-Sondergesandter reist zu Gesprächen nach Tripolis
Picha: Getty Images/AFP/M. Turkia

Mkutano huo juu ya mustakabali wa Libya uliyofanyika mjini Paris hii leo uliowaleta pamoja Kamanda wa eneo la Mashariki  Khalifa Haftar, Waziri Mkuu wa Tripoli Fayez Seraj, na viongozi wa mabunge mawili hasimu unanuia kuwahimiza kukubaliana juu ya kanuni ya kumaliza mgogoro na kusonga mbele katika kuandaa uchaguzi wa Kitaifa.

Waziri Mkuu wa Tripoli Fayez Seraj, amesema kushiriki kwa pande zote zinazohusika katika mgogoro wa Libya kunaonyesha nia ya kweli ya kupata suluhisho la kisasa.

Kamanda wa eneo la Mashariki Khalifa Haftar,Picha: picture alliance/dpa/M. Elshaiky

Taarifa ya pamoja iliyotolewa imesema kwamba pande zote zina nia ya kufanya kazi na Umoja wa Mataifa kufanikisha zoezi la uchaguzi uliyo wa amani na kuaminika pamoja na kuheshimu matokeo ya uchaguzi huo.

Taarifa hiyo imeendelea kusema kwamba pande zote zina nia ya kufungua njia ya kikatiba ya kuandaa uchaguzi na kuwa na sheria zinazohitajika  za uchaguzi ifikapo tarehe 16 mwezi Septemba ili kuandaa uchaguzi wa bunge na wa rais ifikapo Desemba 10 mwaka huu.

Rais Emmanuel Macron asema makubaliano yaliofikiwa ni hatua muhimu kwa  Libya

Hata hivyo makubaliano hayakutiwa saini kama ilivyokuwa imepangiwa hapo awali. Makubaliano hayo yanatoa wito wa kuungana hara kwa benki kuu na kuondokana na serikali  mbili pamoja na taasisi. Pia yameonyesha nia ya kuunga mkono uundwaji wa jeshi la kitaifa na kuhamasishamazungumzo juu ya suala hilo yatakayofanyika mjini Cairo.

Mataifa kadhaa yakiwemo mataifa matano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na pia Italia, Uturuki, Umoja wa falme za kiarabu na Qatar na nchi zilizo jirani na  na Libya walihudhuria mkutano huo.

Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: picture alliance/AP Photo

Chini ya Utawala wa rais Emmanuel Macron, Ufaransa umejaribu kuwa na jukumu kubwa la kushawishi pande hasimu kumaliza mgogoro uliyosababisha kuimarika kwa wanamgambo wa kiislamu.

Rais huyo wa Ufaransa aliwaambia waandishi habari kuwa makubaliano yaliofikiwa ni hatua muhimu kwa  Libya huku akiongeza kuwa ni mara ya kwanza viongozi wa Libya wamekubali kufanya kazi pamoja na kuidhinisha taarifa ya pamoja.

Libya taifa hilo linalotoa mafuta kwa wingi liligawika mwaka 2011 kufuatia uasi uliyofanwa na jeshi la kujihami NATO lililomuondoa Muammar Gaddafi madarakani, na kuanzia mwaka 2014 limekuwa likishindana kati ya makundi mawili ya kisiasa na kijeshi yaliyoko mjini Tripoli na maene ya Mashariki.

Mwandishi: Amina Abubakar/ Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW