1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahasimu wa Netanyahu wakubaliana kuunda serikali

3 Juni 2021

Viongozi wa upinzani nchini Israel wametangaza kufikia makubalino ya kuunda serikali mpya ya mseto hatua itakayofungua njia ya kumuondoa madarakani waziri mkuu wa muda mrefu wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu.

Jair Lapid
Kiongozi wa Upinzani nchini Israel Yair Lapid Picha: Debbie Hill/AP Photo/picture alliance

Tangazo hilo kutoka kwa kiongozi wa upinzani Yair Lapid na mshirika wake Naftali Bennett lilitolewa muda mfupi kabla ya saa sita usiku wa kuamkia leo na kufanikisha kuzuia Israel kuingia kwenye uchaguzi wa tano ndani ya kipindi cha miaka miwili.

Lapid ameandika kupitia ukurasa wa Twitter kuwa serikali hiyo mpya itafanya kazi kwa ajili ya raia wote wa Israel na itafanya kila linalowezekana kuwaunganisha watu wa taifa hilo.

Jumapili iliyopita  Lapid, mtangazaji wa zamani wa televisheni anayeongoza chama cha siasa za wastani cha Yesh Atid alipata uungaji mkono muhimu kutoka kwa Bennett ambaye ni kiongozi wa chama mrengo wa kulia cha Yamina.

Makubaliano kusubiri idhini ya Bunge 

Kiongozi wa chama cha Yamina, Naftali BennetPicha: picture-alliance/dpa

Chini ya makubaliano yaliyofikiwa, Lapid na mshirika wake Bennett watapokezana wadhifa wa Waziri Mkuu kwa Benett kuhudumu kwa miaka miwili ya mwanzo na Lapid ataongoza miaka miwili ya mwisho ya muhula wa miaka minne.

Hata hivyo makubaliano hayo yatahitaji kwanza kuthibitishwa na bunge la nchi hiyo Knesset katika kura inayotarajiwa wiki ijayo.

Iwapo hatua hiyo itapitishwa Lapid na washirika wake watafanikiwa kumaliza enzi ya Benjamin Netanyahu madarakani  ambaye amekuwa waziri mkuu wa Israel kwa miaka 12.

Netanyahu, ambaye anapambana kufa na kupona kubakia madarakani wakati akikabiliwa na kesi ya rushwa anatarajiwa kufanya kila awezalo katika siku zinazokuja kuhakikisha muungano huo mpya hautachukua mamlaka.

Wafuasi wa Netanyahu na Upinzani wapigana vijembe 

Tangazo la kupatikana makubaliano ya kuundwa serikali limezusha hisia mseto na hata vita vya maneno kati ya wafuasi wa waziri mkuu Netanyahu na wale wanaounga mkono upande wa upinzani.

Waandamanaji kutoka pande zote mbili walikusanyika katikati ya mji mkuu wa Israel ambako viongozi wa upinzani walikuwa wakifanya majadiliano ya kuunda serikali ya pamoja.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Picha: Yonatan Sindel/AFP

Mmoja ya wafuasi wa upinzani alisema "Sisi ndiyo washindi rafiki yangu. Sisi ni washindi. Tunashinda. Tumeshinda pambano hili. Tulishinda uchaguzi. Hatimaye tumepata serikali."

Hata hivyo wafuasi wa Netanyahu nao hawakuwa nyuma kumpigia debe mwanasiasa huyo na kufanya kejeli kuwa muungano wa upinzani hautavuka vigingi.

"Wiki moja na nusu ijayo hakutakuwa na serikali iliyopigiwa kura kwenye Knesset. Zingatia maneno yangu ninakwambia wiki moja na nusu baadaye hakutakuwa na serikali. Watapambana wenyewe kwa wenyewe na hakutakuwa na serikali." amesema mfuasi huyo wa Netanyahu.

Katika uchaguzi wa mwezi Machi chama cha Netanyahu cha Likud kilipata wingi wa viti bungeni lakini idadi yake haikutosha kumwezesha kuunda serikali na washirika wake wa vyama vidogo walikataa kuungana kupata wingi ndani ya Bunge.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW