Mahasimu wa Yemen watakiwa kufikia maridhiano
9 Mei 2016Wito ulitolewa na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen Ismail Ould Sheikh Ahmed Jumatatu (09.05.2016) umekuja baada ya kuvunjika kwa mazungumzo ya ana kwa ana wakati ujumbe wa serikali ukilalamika kutokuwepo kwa maendeleo katika mazungumzo hayo na waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran wakipinga kuendelea kwa mashambulizi ya anga ya muungano unaongozwa na Saudi Arabia.
Baada ya kuwa na mikutano katika nyakati tafauti na ujumbe wa kila upande ,Ould Sheikh Ahmed amezitaka pande hizo mbili kufikia maridhiano ili kupata ufumbuzi kabambe wa amani kukomesha mzozo huo unaosababisha maafa.
Amesema katika taarifa kwamba washiriki katika mazungumzo ya Kuwait lazima wazingatie matakwa ya wananchi wa Yeman wanaotaka kukomeshwa kwa mzozo huo.
Mikutano yote ya ana kwa ana iliokuwa imepangwa kufanyika hapo Jumapili imeahirishwa na mjumbe huyo amesema mikutano hiyo itafanyika Jumatatu na kuwasihi washiriki watowe ushirikiano wao.
Watupiana lawama
Wajumbe wa pande hizo mbili zinazohasimiana pia wamekutana na waziri wa mambo ya nje wa Kuwait Sheikh Sabah Khaled al-Sabah na mabalozi wa nchi 18 takriban zote zikiwa ni za magharibi zenye kuunga mkono mazungumzo hayo katika juhudi za kuwarudisha tena mahasimu hao wa Yemen katika meza ya mazungumzo.
Waziri wa mambo ya nje wa Yemen amesema mazungumzo hayo yaliyoanza Aprili 21 hayakupiga hatua yoyote ile.Abdulmalek al-Makhlafi anayeongoza ujumbe wa serikali amesema kwa matlaba ya amani wamekubali mapendekezo yote yaliowasilishwa kwao ili waweze kusonga mbele.
Makhlafi amendika kwenye mtandao wa Twitter kwamba lakini baada ya wiki tatu hawana kitu mikononi mwao kwa sababu upande wa pili umekenguka ahadi zake zote.
Kwa mujibu wa duru zilio karibu na waasi upande huo umepinga vikali kwa mjumbe wa Umoja wa Mataifa kile kinachodaiwa kuwa mashambulizi ya muungano unaongozwa na Saudi Arabia hapo Jumapili yaliyouwa watu kadhaa.Hata hivyo hakuna uthibitisho iliopatikana mara moja juu ya mashambulizi hayo ya anga.
Raia wanaotokea kaskazini watimuliwa Aden
Hapo Jumapili serikali inayotambuliwa kimataifa ya nchi hiyo imelaani kutimuliwa kwa mamia ya raia kutoka kwenye mji wa kusini wa Aden ambao imeutangaza kuwa mji mkuu wake wa muda.
Rais Abd Rabu Mansour Hadi ameamuru kusitishwa kutimuliwa huko kwa raia wanaotokea majimbo ya kaskazini nchini Yemen na kurudishwa kwa wale ambao yatari wamefukuzwa.
Vikosi vya usalama hapo Jumamosi viliwakusanya na kuwatimua mamia ya raia wanaotokea Yemen ya kaskazini ambayo kwa sehemu kubwa inadhibitiwa na waasi wa Kihouthi.
Inaelezwa kwamba makundi yenye silaha yanayounga mkono serikali yamekuwa yakiwakamata na kuwahamisha watu kuwapeleka Yemen kaskazini.Maafisa wanasema makundi hayo yamekuwa yakivamia maduka, mikahawa na nyumba na kuwakamata zaidi ya raia 2,000 wanaotokea kaskazini ambao wanasema ni tishio kwa "usalama."
Maafisa wanasema wanatuhumu kutimuliwa kunafanywa na wanaharakati wanaotaka kujitenga ambao wanataka Yemen kusini ijitenge na kaskazini ambayo imeungana nayo hapo mwaka 1990.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa
Mhariri :Iddi Ssessanga