Mahmoud Abbas: Acheni kuipatia Israel silaha
27 Septemba 2024Mkutano huo wa mjini New York kwa kiasi kikubwa umetawaliwa na wasiwasi kuhusu vita vya Urusi nchini Ukraine, vita vya Israel na Hamas huko Gaza, na uwezekano wa kutanuka kwa mzozo wa Lebanon.
Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuacha kuipatia silaha Israel: "Acheni uhalifu huu. Acheni sasa. Acheni kuua watoto na wanawake. Acheni mauaji ya halaiki. Acheni kupeleka silaha kwa Israel. Janga hili haliwezi kuendelea. Dunia nzima inahusika na kile kinachotokea kwa watu wetu huko Gaza na Ukingo wa Magharibi."
Soma pia: Ulimwengu wataka Mashariki ya Kati isitumbukie vitani
Rais Abbas ambaye hata hivyo haliwakilishi eneo la Gaza amesema Wapalestina wanakabiliwa na moja ya uhalifu mbaya zaidi wa zama hizi na kusisitiza kuwa Israel inaendesha uhalifu wa vita kamili na mauaji ya kimbari. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anatarajiwa kulihutubia Baraza hilo leo Ijumaa.
Ama Mkuu wa serikali iliyo uhamishoni na inayotambuliwa kimataifa ya Yemen, Rashad al-Alimi, amesema kuvimaliza vita vya Gaza ni 'hatua ya kwanza' ya kuwatokomeza washirika wa Iran.
Katika hotuba yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, al-Alimi amesisitiza kuhusu umuhimu wa kuzuia mtiririko wa silaha za Iran na kuzuia vyanzo vya fedha kuelekea kwa waasi wa Houthi ambao wamechukua udhibiti wa sehemu kubwa ya Yemen huku akionya kuhusu jukumu la Iran katika kuyumbisha usalama wa Yemen na kanda nzima ya Mashariki ya Kati.
Viongozi wa Kenya na Sudan wahutubia pia
Rais wa Kenya William Ruto ameliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba kufikia Januari mwaka ujao, nchi yake itatuma maafisa zaidi wa polisi nchini Haiti hadi kukamilisha kikosi cha maafisa 2,500.
Ruto alitumia hotuba yake kuomba ufadhili zaidi ili kuunga mkono kikosi hicho cha kupambana na uvunjaji wa sheria ulioenea na kuisaidia nchi hiyo ya Carribean kukabiliana na ghasia za magenge ya wahalifu ambao kwa sasa wanadhibiti asilimia 80 ya mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince.
Aidha, Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan, alipohutubia Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amesema "wamefanya kila waliwezalo ili kukomesha vita vinavyoendelea na uharibifu unaofanywa na wanamgambo ambao amesema wanazuia juhudi za amani.
Al-Burhan amelitolea pia wito baraza hilo kuitambua RSF kama kundi la kigaidi, akisema wanaenedesha mauaji ya kikabila, kuwalazimisha watu kuyahama makazi yao pamoja na mauaji ya halaiki.
Soma pia: Jeshi Sudan laanzisha mashambulizi ya makubwa mji mkuu
Kwa upande wake, Mkuu wa kikosi cha RSF Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana pia kama Hemedti, aliliambia baraza hilo kupitia video iliyorekodiwa kwamba kundi hilo liko tayari kutekeleza mpango wa usitishaji vita kote nchini Sudan ili kuruhusu utoaji wa misaada ya kibinadamu.
Hotuba zingine zilizofuata ikiwemo ya rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel ziligusia pia vita vya Ukraine, mashariki ya Kati, usawa baina ya jamii na changamoto zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi.
Mikutano ya pembezoni mwa hadhara kuu ya UN
Hata hivyo, pembezoni mwa mkutano huo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, viongozi mbalimbali wa dunia wamekuwa wakikutana katika mazungumzo ya kidiplomasia. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alikutana jana na rais wa Marekani Joe Biden katika Ikulu ya White House na kuwasilisha kile kinachojulikana kama "mpango wake wa ushindi" baada ya Biden kutangaza ongezeko la dola bilioni 8 za msaada wa kijeshi kwa Ukraine.
Soma pia: Biden awaalika viongozi wa dunia kuhudhuria mkutano kuhusu Ukraine
Lakini ziara ya Zelensky imegubikwa na mvutano mkali kati yake na mgombea urais wa chama cha Republican, Donald Trump, jambo ambalo linadhihirisha ni jinsi gani uchaguzi wa Marekani wa mwezi Novemba unavyoweza kutatiza uungwaji mkono ambao Kyiv inaupata kwa sasa kutoka kwa mfadhili wake mkuu.
Alipokuwa akimkaribisha Zelensky, Biden alimuhakikishia kuwa "Urusi haitashinda na Ukraine itashinda, na kwamba wataendelea kusimama na Ukraine kila hatua." Kauli kama hiyo imetolewa pia na mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Democratic Kamala Harris ambaye amemueleza Zelensky kuwa msaada wake kwa watu wa Ukraine hautetereki.
Vyanzo: (AP, Reuters, DPAE, AFP)