1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahmoud Abbas aikosoa vikali Israel kwa vitendo vyake Gaza

25 Septemba 2025

Rais wa Palestina amelihutubia baraza hilo kwa njia ya video na kuikosoa vikali Israel kwa vita vyake huko Gaza na kwa vitendo vyake katika eneo Ukingo wa Magaharibi, huku pia akitoa lawama kwa kundi la Hamas.

2025 I Mahmoud Abbas
Rais wa Palestina ameuhutubia Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mtaifa kwa njia ya video na kuikosoa vikali Israel kwa vita vyake huko GazaPicha: Zain Jaafar/AFP/Getty Images

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas amelihutubia baraza hilo kwa njia ya video na kuikosoa vikali Israel kwa vita vyake huko Gaza na kwa vitendo vyake katika eneo Ukingo wa Magaharibi, huku pia akitoa lawama kwa kundi la wanamgambo wa Hamas.

Kama ilivyotarajiwa, hotuba hiyo ya Abbas katika Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ilisubiriwa kwa hamu na wengi miongoni mwa mataifa wanachama wa Umoja huo, wengi wao ambao kwa sasa wameamua tayari kuitambua Palestina kama taifa huru.

Katika hotuba hiyo aliyoitoa kwa njia ya video kutokana na kunyimwa viza na Marekani ya kuingia nchini humo na kuhudhuria mkutano huo,  Abbas amesema watu katika Ukanda waGaza wanakabiliwa na mauaji ya halaiki, njaa, na uharibifu mkubwa.

Kiongozi huyo amesema vitendo vinavyofanywa na majeshi ya Israel huko Gaza ni moja ya matukio ya kutisha zaidi pengine kuliko matukio yote yaliyotokea katika karne ya 20 na 21.

Rais wa Palestina Mahmoud PalestinaPicha: Jeenah Moon/REUTERS

"Inachofanya Israel sio tu uchokozi, bali ni uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, itakumbukwa na kufuatiliwa. Itarekodiwa katika vitabu vya historia na dhamiri ya kimataifa kama mojawapo ya matukio ya kutisha zaidi ya maafa ya mwanadamu katika karne ya 20 na 21."amesema Abbas.

Kuhusu kundi laHamas,  kiongozi huyo ametoa lawama za waziwazi kwa kundi hilo na kusema kwamba hakutakuwa na nafasi yeyote kwa Hamas kuitawala Gaza tena baada ya vita.

Abbas: Muendelee kuitambua Palestina kama taifa huru

Mahmoud Abbas ametoa wito pia kwa nchi zote wanachama wa umoja huo kuendelea kuitambua Palestina kama taifa huru huku akiuhakikishia ulimwengu kuwa yuko tayari kushirikiana na Marekani, Saudi Arabia na Umoja wa Mataifa katika kufanikisha mpango wa amani huko Mashariki ya Kati.

Ikumbukwe kwamba hotuba hii inakuja siku tatu baada ya mataifa ya magharibi ya Ufaransa, Canada na Uingereza kuchukuwa hatua ya kulitambua taifa la Wapalestina. 

Rais wa Palestina Mahmoud AbbasPicha: Richard Drew/AP Photo/picture alliance

Baada ya hotuba hiyo ya Abbas, kesho ni zamu ya Waziri Mkuu wa Israel,Benjamin Netanyahu kutoa hotuba katika mkutano huo ambapo anatarajiwa naye kuelezea msimamo wa nchi yake kwa vita vya huko Gaza.

Viongozi wengine wanaotoa hotuba zao jioni hii ni pamoja na Rais wa Baraza la Ulaya Antonio Costa na mawaziri wakuu wa mataifa ya Ubelgiji, Italia na Uholanzi.

Mzozo huu wa Mashariki ya Kati pamoja na vita vyaUrusi dhidi ya Ukraine ni miongoni mwa mada kuu katika mkutano huu unaondelea hadi siku ya Jumatatu ya wiki ijayo.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW