1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waumini wa Kiislamu wakusanyika Saudi Arabia kwa Hija

17 Agosti 2018

Hija ambayo ni mojawapo ya nguzo tano za Kiislamu itaanza jioni ya tarehe 19 ambayo ni Jumapili na kukamilika tarehe 24 Ijumaa wiki ijayo. Kila Muislamu hutakiwa kuifanya angalau mara moja katika maisha yake.

Saudi-Arabien Moslem-Pilger in Mekka
Kaaba, eneo takatifu ambalo huzungukwa na waumini wa Kiislamu wanapofanya ibada wakati wa HijaPicha: Getty Images/AFP/K. Sahib

Waumini milioni mbili wa dini ya Kiislamu watakusanyika nchini Saudi Arabia wiki hii kwa ibada ya Hija ambayo hufanyika kila mwaka. Kufikia jana waumini milioni 1.6 walikuwa tayari wamewasili nchini humo kwa ibada hiyo. Maelefu walionekana wakifika katika mji wa Makka, huku makundi kutoka mataifa mbalimbali yakiwa yamevalia nguo za  rangi tofauti kuwatofautisha.

Baadhi walionekana wakiwasukuma kwa viti vya magurudumu wazee ambao ni jamaa zao, na wengine kuwapigia waliowaacha nyumbani kupitia video, mbali na baadhi kununua barafu kutokana na joto kali linaloshuhudiwa  nchini humo. Kwa wengi, hii ni mara yao ya kwanza kufika nchini humo kwa hija. Bila kuzingatia kabila au taifa analotoka mtu, hija huanza kwa ´´Ihram´´, kuvalia vazi jeupe kuanzia juu hadi chini. Kwa wanaume, ni kanzu nyeupe inayovaliwa kwa suruali nyeupe ndani. Wanawake huvalia nguo ndefu nyeupe ambayo huacha uso na mikono pekee ikionekana.

Kisha mahujaji hufanya ibada kwa kuizunguka Kaaba na katika Mlima Arafat ulioko Mashariki ya mji wa Makka. Hija hukamilika kwa kuadhimishwa kwa siku kuu ya Eid al-Adha, ambayo husherehekewa kwa siku tatu na walioko Makka huanza Eid kwa kumpiga mawe shetani. Eid al-Adha vile vile inahusisha kuchinjwa kwa kondoo, na nyama yake kugawanyiwa Waislamu wasiojiweza.

Picha: Getty Images/AFP/Y. Al-Zayya

Wanyama wengine ambao huchinjwa na waislamu waliosalia nyumbani ni mbuzi na ng´ombe au kwa wengine kuku. Hatua hiyo inaashiria kujitolewa kwa Nabii Ibrahim kumtoa sadaka mwanawe wa kiume, Ismael, kufuatia na agizo la Mwenyezi Mungu.  Ibada ya Hija hata hivyo imezipa changamoto za usafirishaji na vifaa idara mbalimbali nchini Saudi Arabia.

Kituo cha Utafiti cha Pew kimesema kwamba idadi ya waumini wa Kiislamu itaongezeka kutoka watu bilioni 1.8 mwaka 2015 hadi watu bilioni tatu ifikapo mwaka 2060. Mwaka huu Wasaudi wamezindua mpango kwa jina ´´Smart Hajj´´ huku kukiwa na program mbalimbali za kuwasaidia mahujaji na kila kitu wanachohitaji ikiwamo mipango ya usafiri na huduma za matibabu.

Mojawapo ya program hizo kwa jina Asefny, kwa mfano ilizinduliwa na Shirika la Hilali Nyekundu la Saudi Arabia kuwasaidia mahujaji wanapohitaji huduma za dharura za afya. Idara za afya zitaweza kuwatambua wanaohitaji huduma hizo kupitia program hiyo. Aidha Wizara ya Mambo ya Hija nchini humo inasimamia programu inayojulikana kama Manasikana, ambayo inatoa tafsiri kwa mahujaji ambao hawazungumzi lugha za Kiarabu wala Kiingereza.

Hija ya mwaka huu inajiri wakati ambapo taifa hilo linaendesha ukandamizaji dhidi ya upinzani wa kisiasa, na utawala wake ukiendelea kutekeleza kampeni ya kuboresha taswira yake kama mojawapo ya mataifa yenye udhibiti mkali. Vile vile inajiri zaidi ya mwaka mmoja baada ya kuzuka mgogoro mkubwa wa kisiasa katika ghuba hiyo, unaozipambanisha Saudi Arabia na Qatar.

Saudi Arabia, ambayo ni msafirishaji mkubwa wa mafuta, pamoja na washirika wake, wanailaumu Qatar kwa kuyaunga mkono makundi ya Kisunni ya itikadi kali pamoja na Iran ambayo ni hasimu mkubwa wa Saudi Arabia. Wamesitisha uhusiano na Qatar na kukomesha safari zote za ndege kutoka au kuingia mjini Doha. Hata hivyo Qatar inakana madai hayo.

Mahujaji kutoka Iran pia wamefika nchini humo kwa ibada ya Hija. Awali Tehran ilikuwa imesitisha mpango wa kuwapeleka raia wake kuhiji kufuatia mkanyagano ulioshuhudiwa mwaka 2015 ambapo mahujaji 2,300 walifariki dunia, wakiwamo mamia ya raia wa Iran.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/AFPE

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW