Mahusiano Kati ya Bayern na Dortmund yameganda
25 Aprili 2014Kwa nini? Siyo usajili wa wachezaji tu..hapana. Ni kwa sababu ya mzozo wa deni linalotokana na mkopo uliodumu mwongo mmoja.
Timu hizo mbili zimekuwa zikishambuliana kwa maneno kuhusiana na mkopo wa kiasi cha euro milioni mbili ambao Bayern iliwapa Dortmund wakati walipokuwa wamekabiliwa na matatizo ya kifedha mwaka wa 2004.
Rais wa Bayern Karl Hopfner anadai Afisa Mkuu Mtendaji wa Dortmund Hans-Joachim Watzke hakusema ukweli alipodai kuwa Bayern wanadai kupewa kiasi kikubwa cha riba kutokana na mkopo huo.
Katika misimu minne iliyopita, Dortmund wameibuka kuwa wapinzani wakuu wa Bayern katika ligi ya nyumbani na Ulaya, huku wakishinda mataji mawili katika mwaka wa 2012 na ligi 2011 kabla ya kushindwa na mahasimu hao wa Munich katika fainali ya Champions League msimu uliopita.
Hata hivyo wamewapiga Bayern magoli matatu kwa sifuri katika Bundesliga hivi majuzi ili kujirejeshea hadhi yao. Afisa Mkuu Mtendaji wa Bayern Karl Heinz Rummenige anasema Bayern haihitaji mkutano wa kilele wa amani na wala haihitaji mkutano wowote na Dortmund.
Bayern ambao wanalenga kurudia mafanikio ya msimu uliopita kwa kushinda mataji matatu, Bundesliga, Champions League na kombe la DFB, wanapambana na Real Madrid Jumanne ijayo katika pambano la marudiano la nusu fainali.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman