1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahusiano ya Marekani, Urusi yafikia kiwango cha chini

13 Aprili 2017

Marais wa Marekani na Urusi wametoa kauli zilizodhihirisha kuwa mahusiano kati ya nchi zao yamefikia kiwango cha chini kabisa. Hayo ni wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani akiwa ziarani Moscow

Russland Rex Tillerson und Sergey Lavrov
Picha: picture alliance/Sputnik/R. Sitdikov

Mjini Washington, Rais Donald Trump alisema kuwa mahusiano kati ya Marekani na Urusi yamefikia kiwango cha chini kabisaa. "Lingeweza kuwa jambo zuri kama tutashirikiana na Putin na kama tutashirikiana na Urusi. Na hilo huenda likafanyika, na huenda lisifanyike. huenda likawa tu kinyume chake".

Saa chache kabla, Rais wa Urusi Vladmir Putin naye pia alielezea mashaka, akisema katika mahojiano na televisheni  ya Urusi, kuwa "kiwango cha uaminifu hasa katika ngazi ya kijeshi, hakijaimarika bali kimezorota."

Kauli za marais hao wawili zilikuja wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson akipata mapokezi yasiyo ya kawaida ya kiuadui mjini Moscow, ambako matumaini yoyote kuwa utawala wa Trump ungepunguza mahusiano yenye majibizano yalivunjika wiki hii baada ya shambulizi la kombora la Marekani nchini Syria.

Rais Putin ni mshirika wa karibu wa AssadPicha: picture alliance/dpa/A. Druzhinin

Tillerson alikutana na Putin katika ikulu ya Kremlin baada ya kuzungumza na waziri mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov, kwa karibu saa tatu. Marekani inaituhumu Urusi kwa kujaribu kuficha matumizi ya Assad ya silaha za sumu baada ya shambulizi la wiki iliyopita katika mji Khan Sheikhoun unaodhibitiwa na waasi nchini Syria na kusababisha vifo vya karibu watu 90.

Urusi imesimama na Assad, ikisema gesi hiyo ya sumu ilitumiwa na waasi, kauli ambayo Marekani inakanusha ikisema sio ya kweli. Tillerson alirudia msimamo wa Marekani kuwa Assad lazima aachie madaraka "Tunadhani kuwa ni muhimu kuwa kuondoka kwa Assad kufanywe katika njia ya mpangilio, ili maslahi fulani na watu anaowawakilisha wajihisi kuwa wamewakilishwa katika meza ya mazungumzo kwa ajili ya suluhisho la kisiasa".

Lakini Lavrov alisema hatua kadhaa zilipigwa kuhusu Syria katika mkutano wake na Tillerson, na kuwa jopokazi litaundwa ili kutathmni hali mbaya ya mahusiano ya Marekani na Urusi. "Licha ya matatizo kadhaa yaliyopo, iwe ni ya kimalengo na ya kujitungia, kuna uwezekano mdogo wa ushirikiano na Urusi iko wazi kwa hilo".

Trump alibadilisha msimamo wake kuhusu NATOPicha: Reuters/J. Ernst

Urusi hapo jana ilipinga kwa kutumia kura yake ya turufu azimio la nchi za Magharibi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililonuia kulaani sambulizi la gesi ya sumu na kumshinikiza Assad kushirikiana na uchunguzi wa kimataifa kuhusiana na shambulizi hilo.

Katika hatua nyingine inayoweza kuathiri zaidi mahusiano na Urusi, Trump amesema kuwa Jumuiya ya Kujihami ya NATO haijapitwa na wakati, kama alivyokuwa ametangaza wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka jana. Lakini alisema jana katika kikao cha wanahabari katika Ikulu ya White House na Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg kuwa wanachama wa jumuiya hiyo ya kijeshi bado wanastahili kulipa kiwango chao cha mchango kwa muungano huo wa usalama wa mataifa ya Magaharibi.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW