Maiz yapunguzwa kasi katika Bundesliga
18 Oktoba 2010Kabla ya pambano hilo Maiz iliwaduwaza washabiki wa kabumbu kwa kushinda mechi saba mfululizo ikiwemo dhidi ya mabingwa watetezi Bayern Munich.Mashuti ya Marco Caligiuri wa Mainz na Ze Roberto wa Hamburg yaligonga mwamba huku bao la Ruud van Nisterooy wa Hamburg likikatiliwa, kabla ya Guerrero kufunga bao hilo.Hataha hivyo lakini Hamburg Armin Veh aliisifu Mainz.
Kipigo ambacho Mainz ilikipata, kilitoa nafasi kwa Borussia Drtmund kuchukua usukani wa Bundesliga, baada ya kufanikiwa kuwachapa mahasimu wao FC Cologne, mabao 2-1.Ilionekana dhahiri pambano hilo lingemalizika kwa sare ya bao 1-1, baada ya Lucas Podoski kusawazisha bao la Dortmund katika dakika ya 82, lakini mabeki wa FC Cologne walizubaa na kutoa nafasi kwa Nuri Sahin kufunga bao la ushindi sekunde chache kabla ya mpira kumalizika.Dortmund na Mainz zote zina pointi 21 lakini Dortmund wana mabao mengi.
Kwa upande mwengine, balaa la kuwa na mejeruhi wengi,linalowakabili mabingwa watetezi Bayern Munich lilitoa nafasi kwa Mario Gomez kuchomoza makucha yake, na kuifufua kutoka kaburini Bayern pale alipopachika mabao matatu pekee yake dhidi ya Hanover 96.
Gomez mshambuliaji ghali katika Bundesliga aliyenunuliwa kutoka Stuttgart kwa kitita cha Euro millioni 30 msimu huu, amekuwa hana nafasi katika kikosi cha kwanza cha Bayern chini kocha Louis van Gaal.Lakini kiwango alichokionesha mwishoni mwa wiki kimemkosha kila mtu.
Katika mechi nyingine za Bundesliga, Hoffenheim ikiwa nyumbani ilibidi kufanya kazi ya ziada kuweza kuifunga Borussia Moenchgladbach mabao 3-2 na kuchupa hadi katika nafasi ya nne, nyuma ya Bayer Leverkusen yenye pointi 15 ambayo ilitamba ugenini kwa kuifunga Wolfsburg mabao 3-2.
Timu iliyopanda daraja msimu huu Kaiserslautern ilikiona cha moto tena nyumbani kwake pale ilipocharazwa mabao 3-0 na Eintracht Frankfurt, huku Werder Bremen ikimtuliza shetani kichwani baada ya kupepesuka katika mechi zilizopita, kwa kuichapa Freiburg mabao 2-1.
Mpaka sasa mgiriki Theofanis Gekas wa Frankfurt pamoja na Papiss Cisse wa Freiburg wanaogoza Bundesliga katika upachikaji wa mabao, baada ya kuzifumania nyavu mara saba kila mmoja.
Ama huko nchini Uingereza katika Premier League, bundi aliendelea kulia katika paa la Liverpool pale walipochapwa na mahasimu wao wakubwa Everton mabao 2-0, kipigo kilichoshuhudiwa na wamiliki wapya wa Liverpool John W Henry na Tom Werner.
Liverpool sasa inachungulia kaburi kwani inaisaidia West Ham United kukamata nanga ya ligi hiyo, zote zikiwa na pointi sita kila mmoja pamoja na Wolverhamton.
AFRIKA
Tuelekee sasa barani Afrika, ambako klabu bingwa ya ligi ya mabingwa wa soka barani humo, TP Englebert Mazembe, imefanikiwa kuingia fainali baada ya kutoka suluhu bin suluhu ugenini na JS Kabylie ya Algeria kwani katika mechi ya kwanza mjini Lubumbashi ilishinda kwa mabao 3-1.Sasa Mazembe itapambana na Esperance ya Tunisia iliyoindosha Al Ahly ya Misri kwa bao la ugenini.
Tukielekea Afrika mashariki, Timu ya taifa ya wanawake ya kandanda ya Tanzania iko katika mawindo makali kwa ajili ya fainali za kombe la mataifa ya Afrika kwa wanawake zitakoanza mwishoni mwa mwezi huu nchini Afrika Kusini.Tanzania nchi pekee kutoka Afrika Mashariki na Kati inayoshiriki fainali hizo imepangwa pamoja na wenyeji Afrika Kusini, Mali na Nigeria.
Kocha wa Timu hiyo Charles Boniface Mkwasa amesema ana matumaini na vijana wake.
Nchini Kenya katika ligi ya kabumbu Ulinzi ilijikuta ikishindwa kupanua mwanya zaidi wa kukaa kileleni kwa pointi nane, baada ya kulaziamishwa suluhu bin suluhu na Tusker, huku mabingwa watetezi Sofapaka wakicharuka mbele ya Sony Sugar na kuwachapa mabao 2-0.
Shirikisho la Kabumbu duniani FIFA limesema kuwa, linachunguza ushahidi uliyowasilisha na gazeti la Sunday Times la Uingereza lililodai kuwa wajumbe wawili wa kamati kuu ya shirikisho hilo walipokea mlungula wakati wa zoezi la upigaji kura kuchagua mwenyeji wa fainali za dunia, litakalofanyika mwezi Disemba.
Mwandishi wa gazeti hilo akijifanya mmoja wa wapambe wa kampuni moja la kimarekani linalotaka fainali za kombe hilo zifanyike Marekani, alifanikiwa kuwarekodi wajumbe hao Amos Adamu kutoka Nigeria na Reynald Temarii Rais wa Shirikisho la Soka la Ocenia wakiomba fedha kutoka shirika hilo kufadhili miradi yao.
MASUMBWI
Bingwa wa uzito wa juu duniani anayetambuliwa na Baraza la Masumbwi Duniani WBC Vitalis Klitschko wa Ukraine, jana usiku alifanikiwa kuutetea ubingwa wake kwa kumtwanga kwa pointi Shannon Briggs wa Marekani katika pambano lililofanyika mjini Hamburg hapa Ujerumani.
Hata hivyo Briggs mara baada ya pambano hilo wakati alipokuwa akisubiri kuchukuliwa vipimo vya dawa za kuongeza nguvu, alianguka na kukimbizwa hospitali ambako amewekwa katika chumba cha uangalizi maalum kufuatia kipigo cha Klitscho.
Mwamuzi wa pambano hilo Ian John-Lewis kutoka Uingereza amesukumiziwa lawama, kwa kushindwa kumuokoa Briggs baada ya kuwa amejeruhiwa vibaya na makonde ya Klitscho na kumuacha kuendelea na pambano hadi mwisho.
RIADHA
Naye mwanariadha wa Kenya Vincent Kiplagat jana liweka rekodi ya kukimbia kwa kasi zaidi katika mbio za nyika huko Istanbul Uturuki baada ya kutumia muda wa saa mbili dakika 10 na sekunde 39. Ashu Kasim wa Ethiopea alishinda mbio hizo kwa upande wa wanawake baada ya kutumia muda wa saa mbili dakika 27 na sekunde 25.
Mwandishi:Aboubakary Liongo
Mhariri:Mohamed Abdulrahman