Majadiliano ya bajeti yakwama
10 Novemba 2012Serikali za mataifa ya umoja huo pamoja na bunge zimeshindwa kupata msimamo wa pamoja kuhusu suala la utendaji baada ya karibu saa nane za mazungumzo jana Ijumaa(09.11.2012).
Pande hizo mbili zitajaribu tena kupata makubaliano siku ya Jumanne, kabla ya muda wa mwisho ambao ni usiku wa manane , kuweza kukubaliana juu ya bajeti ama kuirejesha halmashauri ya Ulaya , katika kazi ya kuipanga upya bajeti hiyo.
Wanasiasa wa umoja wa Ulaya hawatilii manani sana uchelewesho huo, na wana matumaini kuwa muda wa mwisho unaweza kufikiwa.
Jumanne ndio mwisho
"Ni pale tu ambapo hatutaweza kufanikiwa siku ya Jumanne, tuwe watulivu na hatupaswi kujiuliza kuhusu nia njema ya wadau wote," amesema Adreas Mavroyiannis, naibu waziri anayehusika na masuala ya ulaya kutoka Cyprus, nchi ambayo kwa sasa inashikilia urais wa kupokezana wa umoja wa Ulaya.
"Inatokea katika wakati wa muafaka kuwa kuna kuwa na hali ya mkwamo , wasi wasi," amesema kamishna wa bajeti ya umoja wa ulaya Janusz Lewandowski. "lakini nafikiri hali ya uwajibikaji ipo."
Mavroyiannis, hata hivyo , amesema kuwa hali ya kuweza kushindwa siku ya Jumanne "haiwezi kuondolewa kabisa".
Mkwamo ukizidi ni hatari
Kabla ya mazungumzo hayo ya jana Ijumaa(09.11.2012) , maafisa wa serikali za umoja wa Ulaya wameonya kuhusu hatari ya kuendelezwa kwa mazungumzo hayo hadi kuingia katika mwaka 2013, kabla ya kuanza kwa majadiliano juu ya bajeti ya mwaka 2014 hadi 20 katika muda wa wiki mbili.
"nafikiri itatoa ishara mbaya sana iwapo tutaendelea kuvutana kuhusiana na masuala haya," amesema Brian Hayes waziri wa fedha wa Ireland.
Serikali za mataifa ya umoja wa Ulaya pamoja na bunge la Ulaya zinatofautiana kwa mbali sana kuhusiana na kiasi gani kitumiwe mwaka ujao.
Mataifa wanachama yanataka bajezi inayofikia kiasi cha euro bilioni 132.7 ama ongezeko la asilimia 2.8.
Serikali za kihafidhina zinazoangalia sana masuala ya bajeti kama Ujerumani, Uholanzi na Denmark yanasisitiza kuwa kiwango hicho kikubalike, suala ambalo pia linaungwa mkono na Ufaransa na Uhispania, na kuweka mataifa matatu yenye uchumi mkubwa katika umoja wa Ulaya katika upande mmoja.
"Muktadha ni juu ya kubana matumizi. Serikali ya Uhispania inachukua hatua madhubuti za kubana matumizi. Hii ndio sababu ni muhimu kwa umoja wa Ulaya kuchukua juhudi pia, kuanzisha hatua za kupunguza matumizi," balozi wa Uhispania katika umoja wa Ulaya , Alfonso Dastis amesema.
Lakini wabunge wa umoja wa ulaya wanapigia upatu bajeti itakayofikia kiasi cha euro bilioni 137.9, ama ongezeko la asilimia 6.8, wakidai kuwa fedha hizo zinahitajika ili kuweza kugharamia mipango na miradi ambayo imekubalika hapo kabla.
Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Stumai George