Majadiliano ya kuunda serikali kuu ya Muungano
18 Oktoba 2017Tunaanzia lakini Berlin yanakofanyika mazungumzo kati ya wawakilishi wa vyama ndugu vya Christian Democratic Union na Christian Social Union-CDU/CSU, waliberali wa FDP na walinzi wa mazingira die Grüne. Ni mazungumzo magumu na huenda yakadumu muda mrefu linaashiria gazeti la "Rheinpflaz" la mjini Ludwighafen, linalozungumzia vizingiti vinavyowekwa na FDP. Gazeti hilo linaendelea kuandika: "Hata kabla ya mazungumzo kuanza rasmi, kuhusu uwezekano wa kuundwa serikali ya muungano wa Jamaica, Christian Lindner anaanza kujenga ukuta : Wizara ya fedha haistahiki kukabidhiwa chama cha CDU, amesema katika mahojiano na gazeti moja. Watu wanajiuliza kama matamshi hayo yanaweza kupuuzwa au kama ni matamshi ya kiburi. Yanaweza kutafsiriwa kwa namna zote mbili; kwasababu vipi anaweza kuzungumzia nyadhifa kabla ya mada muhimu kufafanuliwa. Ni kiburi kwasababu Christian Lindner hana jukumu la kutoa madai kama hayo. Ikiwa mwenyekiti huyo wa chama cha FDP atatumia sauti hiyo hiyo atakapoingia katika mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano , basi nafasi ya kufanikiwa mazungumzo hayo mtu anaweza kusema itapungua.
Ndoto ya wakurd ya kuwa nan taifa lao itasalia kuwa ndoto
Gazeti la kaskazini mwa Ujerumani, "Hannoversche Allgemeine" linaangalia kishindo kinachowakabili wakurd tangu walipoitisha kura ya maoni ya kudai utawala mkubwa zaidi wa ndani kaskazini mwa Iraq. Gazeti linahofia mvutano kati ya serikali ya mjini Baghdad na ile ya mjini Erbil usije ukasababisha wimbi jengine la wakimbizi kuelekea Ulaya. Gazeti linaendelea kuandika: "Wakurd tangu zamani hawakutendewa ipasavyo; juhudi zao za kupigania uhuru ingawa zinaungwa mkono na baadhi ya nchi za magharibi, hata hivyo juhudi hizo zitasalia kuwa ndoto: Mbali na serikali kuu ya Iraq mjini Baghdad, Uturuki na Iran pia zinapinga moja kwa moja juhudi za Wakurd za kujipatia uhuru wao. Nchi za magharibi zitajiiepusha na kutaka kuutingisha mshikamano wa majirani wa Wakurd. Kura ya maoni ya Wakurd kudai taifa lao haijapokelewa kwa shauku kubwa. Sasa lakini Ujerumani na Ulaya zinakabiliwa na jukumu la upatanishi katika jimbo la Kirkuk.Tena kwa masilahi yao wenyewe. Wengi nchini Iraq wamekimbia vitisho vya wanamgambo wa itikadi kali wa dola la Kiislamu kaskazini mwa Iraq. Pindi mapigano yakiripuka hivi sasa katika eneo hilo kati ya jeshi la Iraq na Wakurd, basi wimbi jengine la wakimbizi litazuka. Na hawatakuwa na lengo jengine isipokuwa Ulaya."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlanadspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga