1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Rwanda kujenga kiwanda cha kutengeneza chanjo ya Covid-19

22 Juni 2021

Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema serikali yake ipo katika maandalizi ya mwisho kujenga kiwanda cha kutengeneza chanjo za magonjwa mbalimbali ikiwemo chanjo dhidi ya Covid-19. Senegal na afrika Kusini pia zinazingatiwa.

Kuba Havana Coronavirus Lockdown
Picha: YAMIL LAGE/AFP via Getty Images

Rais Paul Kagame amesema hayo baada ya kuzungumza katika mkutano wa kimataifa wa jukwaa la kiuchumi nchini Qatar uliofanyika kwa njia ya mtandao.

"Sisi ndiyo tutakuwa ni vituo katika bara zima la Afrika ambapo chanjo hizi zitakuwa zikitengenezwa.," alisema Rais Kagame.

Kagame ametoa taarifa hiyo wakati Rwanda ikikabiliwa na wimbi la tatu la maambukizi ya virus vya Corona ambavyo vimesababisha serikali kuchukua hatua kali hadi sasa.

Soma pia: Rwanda yapokea shenena yake ya chanjo ya corona

Amesema kwa kushirikiana na wadau wengine wa kimataifa maandalizi ya kujenga kiwanda cha kutengeneza chanjo za Covid-19 nchini Rwanda yamefika mbali.

Rais wa Rwanda Paul Kagame. Picha: Presse- und Kommunikationsdienst der Präsidentschaft der DR Kongo

"Tumeshirikiana na viwanda ambavyo vina teknolojia ya juu maaarufu kama MRNA, hii ni teknolojia mpya na ya kisasa ambayo hutumia njia mbalimbali za kutengeneza chanjo za kuzuia hata magonjwa mengine, lakini pia tunazungumza na wadau katika masuala ya fedha na hapa tunasema huenda miezi michache ijayo kuanzia mkasikia taarifa nyingine."

Wimbi la tatu la Covid-19

Rwanda imeendeelea kuchukua mikakati mingine kukabiliana na janga la Covid-19 lakini waziri wa afya wa nchi hiyo Dr Daniel Ngamije anasema hii ni taarifa nzuri kuhusu kukabiliana na ugonjwa wa covid-19 kwa sababu ndiyo suluhisho la mwisho kuhusu janga hili na hata magonjwa mengine ambayo yanaweza kuripuka siku zijazo.

Soma pia:Bara la Afrika linahitaji haraka chanjo za COVID-19 

"Tunaamini kwamba kwa kutumia teknolojia ya MRNA ya chanjo ya Corona na magonjwa mengine, narudia kusema kwa kujenga kiwanda hiki ni habari njema kuhusu kukabiliana na janga hili," amesema waziri Ngamije.

Rais Paul Kagame amesema, kutengeneza chanjo za corona barani Afrika kutasaidia kukabiliana na maambukizi kwa kutoa chanjo nyingine kwa waafrika kama ilivyo katika mataifa yaliyoendelea.

Baadhi ya chanjo za Covid-19Picha: Eibner-Pressefoto/EXPA/Feichter/imago images

"Kwa sasa Afrika inajishulisha sana na kuhakikisha tunapata chanjo za corona na sasa tunaendelea kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha azma hii inafikiwa barani Afrika.

Tunao wale kutoka shirika la fedha ulimwenguni, umoja wa ulaya na wengine na tukimaliza mchakato huu tutaweza kuzitengeneza na kuzipata chanjo hizo kwa wakati kama yalivyo maeneo mengine ulimwenguni," alisema rais wa Rwanda.

Soma pia: Ujerumani kusaidia utengenezaji chanjo Afrika Kusini

Wimbi la tatu la maambukizi ya virusi vya corona limeikumba Rwanda na tayari serikali imeweka mikakati kabambe ya kuzuia safari zote kutokea mji mkuu wa Rwanda, Kigali kuelekea mikoani na kutoka mikoani kuelekea jijini Kigali.

Safari za kati ya wilaya na wilaya pia zimepigwa marufuku na amri ya kutotembea usiku sasa ni kuanzia saa moja za usiku hadi saa kumi alfajiri.

Sylivanus Karemera DW Kigali.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW