1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Majaji kumchunguza Trump kwa jaribio la kupindua uchaguzi

19 Julai 2023

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amesema amepokea barua kutoka kwa wakili Jack Smith inayodai atachunguzwa na jopo la majaji, kuhusiana na juhudi zake za kutaka kupindua matokeo ya uchaguzi wa rais mwaka 2020.

Former US President Donald Trump
Picha: Andy Buchanan/AFP

Trump ameyasema haya wakati ambapo jaji mmoja amedokeza kuwa, huenda kesi ya nyaraka za siri inayomkabili rais huyo wa zamani isianze mwezi Desemba, kama walivyopendekeza waendesha mashtaka.

Trump ameyasema hayo kupitia ujumbe aliouandika kwenye mtandao wake binafsi wa kijamii wa Truth Social. Mawakili wa Trump lakini hawakupatikana kutoa tamko kuhusiana na suala hilo, halikadhalika msemaji katika afisi ya wakili Smith, aliyepewa jukumu la kuyachunguza madai ya Trump.

Barua hiyo ni ishara ya wazi kwamba Trump ambaye yuko mstari wa mbele katika kinyang'anyiro cha kuwania urais mwakani kupitia tiketi ya chama cha Republican, huenda akafunguliwa mashtaka ya jinai kuhusiana na juhudi zake za kutaka kusalia madarakani, hata baada ya kushindwa katika uchaguzi na rais wa sasa Joe Biden.

Kesi kuahirishwa hadi baada ya uchaguzi wa 2024?

Maafisa kadhaa wametoa ushahidi kwamba, katika siku zake za mwisho madarakani,Trump aliwashinikiza na madai ya uongo ya wizi wa kura. Mnamo Januari 6 mwaka 2021, wafuasi wake waliyavamia majengo ya bunge ya Capitol Hill, ili kulizuia bunge kuidhinisha ushindi wa Biden.

Wakili Jack Smith anayeongoza upande wa mashtaka dhidi ya TrumpPicha: Leah Millis/REUTERS

Wakati huo huo, jaji mmoja nchini Marekani amedokeza kwamba huenda mwezi Desemba ikawa ni mapema mno kwa kesi ya jinai inayohusu nyaraka za siri inayomkabili Trump, kuanza kusikilizwa. Jaji Aileen Cannon lakini, hakusema iwapo atakubaliana na ombi la Trump kwamba kesi hiyo iahirishwe mpaka baada ya uchaguzi wa mwaka 2024.

Jaji Cannon amesema atatoa amri karibuni kuhusiana na suala hilo, baada ya karibu masaa mawili ya kusikilizwa kwa mawakili wa pande zote mbili huko Florida, ambapo mawakili wa Trump walishinikiza kusitolewe tarehe maalum ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Mawakili hao wa Trump wanasema, mteja wao hawezi kupata haki kuelekea uchaguzi na wamesisitiza kwamba wanahitaji muda zaidi kuupitia ushahidi na kujiandaa kwa kile wanachokiita, kesi yenye utata.

Kikosi cha mwendesha mashtaka wakili Jack Smith ambacho kinashinikiza kuanza kwa kesi hiyo mwezi Desemba lakini, kimemueleza jaji kuwa kesi hiyo ya Trump haina utata wowote, kwa hiyo hakuna haja ya kuanza kwake kuahirishwa kwa muda mrefu.

Mahasimu wa Trump chama cha Republican wamuunga mkono

Mawakili hao wamekanusha kwamba Trump amefunguliwa mashtaka kwa kuwa anagombea urais. Mwendesha mashtaka David Harbach amesema hakuna ushawishi wa kisiasa katika kesi hiyo.

Ushindi wa Joe Biden una maana kwa demokrasia ulimwenguni?

This browser does not support the audio element.

Kesi hizo zinazomkabili Trump hazijaathiri kivyovyote juhudi zake za kushinda tiketi ya kugombea urais kwa chama cha Republican. Katika miezi michache iliyopita, uongozi wake umeongezeka kwa mujibu wa kura za maoni na mahasimu wake katika kinyang'anyiro hicho wamemuunga mkono pakubwa, licha ya kesi hizo.

Gavana wa Florida Ron DeSantis anayegombea urais kupitia chamacha Republican pia, amejitokeza na kumtetea Trump Jumanne, akisema kuna njama za kisiasa za kumpelekea huyo mpinzani wake, apatikane na hatia ya kujaribu kupindua matokeo ya uchaguzi wa rais mwaka 2020.

Vyanzo: Reuters/APE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW