1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yaeleza wasiwasi kuhusu mlipuko wa Ebola

Michael Kwena
20 Mei 2026

Shirika la Afya Duniani WHO limeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu kasi ya kusambaa kwa mlipuko wa aina adimu ya Ebola mashariki mwa DRC, huku mamlaka zikithibitisha zaidi ya vifo 130 vinavyoshukiwa kuhusishwa na ugonjwa huo.

Kongo Beni Ebola-Opfer
Serikali ya Kongo imeiomba jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada wa kifedha na kiafya ili kusaidia kukabiliana na mlipuko huoPicha: Jerome Delay/AP/picture alliance

Shirika la Afya Duniani WHO limeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu kasi ya kusambaa kwa mlipuko wa aina adimu ya Ebola mashariki mwa DRC, huku mamlaka zikithibitisha zaidi ya vifo 130 vinavyoshukiwa kuhusishwa na ugonjwa huo pamoja na mamia ya maambukizi mapya.

Serikali ya Kongo imeiomba jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada wa kifedha na kiafya ili kusaidia kukabiliana na mlipuko huo wa Kirusi cha Bundibugyo, ambao hadi sasa hauna chanjo wala dawa iliyoidhinishwa rasmi.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema ana wasiwasi mkubwa kuhusu ukubwa na kasi ya kuenea kwa ugonjwa huo, hasa baada ya visa kuthibitishwa katika maeneo ya mijini pamoja na vifo vya wahudumu wa afya. WHO pia imethibitisha kuwa visa viwili vya Ebola, kimoja kikiwa cha kifo, vimegunduliwa nchini Uganda kwa watu waliotoka Kongo.

Hofu ya Ebola

Katika mji wa Bunia ambako kifo cha kwanza kiliripotiwa, wahudumu wa afya waliovaa mavazi maalumu ya kujikinga wanaendelea kutoa huduma huku hofu ikiongezeka miongoni mwa wakazi. Baadhi ya wananchi wanasema tayari wamewahi kushuhudia madhara ya Ebola katika milipuko iliyopita na wana hofu historia inaweza kujirudia.

Afisa wa afya wa Kongo akimpima mgeni joto la mwili kabla ya kumruhusu kuingia hospitalini mjini Goma.Picha: Jospin Mwisha/AFP

Mtaalamu wa virusi katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Tiba ya Kongo, Jean-Jacques Muyembe, amesema Kongo inatarajia kupokea chanjo za majaribio kutoka Marekani na Uingereza kwa ajili ya kupambana na aina mbalimbali za Ebola. Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa majaribio hayo yatahitaji muda kabla ya kuanza kutumika kwa kiwango kikubwa.

Waziri wa Afya wa Kongo Samuel Roger Kamba amesema mlipuko huo unahitaji mshikamano wa kimataifa kwani unaathiri usalama wa afya duniani. Pia ameonya kuwa kupungua kwa misaada ya kimataifa kunadhoofisha uwezo wa wahudumu wa afya na tafiti za kisayansi."Tunahitaji msaada wa kimataifa.

Virusi hivi vinatuathiri sote, hivyo ni jukumu letu sote kusaidiana. Inasikitisha kuona misaada ikipungua, kwa sababu misaada inapopungua, tunabaki na ulinzi mdogo kwa wauguzi na tafiti chache za kisayansi,”alisema.

WHO imeutangaza mlipuko huo kuwa dharura ya afya ya kimataifa inayohitaji mwitikio wa pamoja wa haraka. Misaada na vifaa vya matibabu vinaendelea kupelekwa katika majimbo mawili yaliyoathirika karibu na Uganda, ingawa juhudi hizo zinatatizwa na hali mbaya ya usalama mashariki mwa Kongo ambako baadhi ya maeneo yako chini ya waasi wa M23.

Wataalamu wanapima uwezekano wa kutumia dawa za majaribio kama remdesivir zilzoonesha mafanikio katika majaribio ya wanyama. Picha: Jerome Delay/AP Photo/dpa/picture alliance

Daktari Anne Ancia, anayesimamia timu ya WHO nchini Kongo, amesema hadi sasa bado haijafahamika mgonjwa wa kwanza kabisa wa mlipuko huo alikuwa nani. Pia amesema hata chanjo yoyote itakayoidhinishwa kwa matumizi ya dharura inaweza kuchukua hadi miezi miwili kabla ya kupatikana kwa kiwango kinachohitajika.

Katika maeneo yaliyoathirika, hospitali nyingi zimeelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na Ebola. Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka limesema baadhi ya vituo vya afya havina hata vyumba vya kutenga wagonjwa, huku vituo vingine vikijaa kabisa wagonjwa wanaoshukiwa kuambukizwa.

Mataifa yanatafuta chanjo 

Mlipuko huo pia umeibua mbio mpya za kutafuta chanjo na dawa dhidi ya kirusi cha Ebola cha Bundibugyo. Wanasayansi kadhaa duniani wamekuwa wakitengeneza chanjo za majaribio, zikiwemo chanjo za teknolojia ya mRNA na nyingine zinazofanana na chanjo ya Ervebo inayotumika dhidi ya kirusi aina ya Zaire.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo inatarajia kupokea chanjo za majaribio kutoka Marekani na UingerezaPicha: Sia Kambou/AFP/Getty Images

Mtaalamu wa virusi Thomas Geisbert amesema tayari kuna chanjo ya sindano moja dhidi ya Bundibugyo Ebola iliyofanyiwa majaribio kwa nyani na kuonyesha matokeo mazuri. Hata hivyo, amesema changamoto kubwa ni ukosefu wa uwekezaji kutoka kampuni kubwa za dawa kwa sababu soko la chanjo hiyo halionekani kuwa na faida kubwa kibiashara.

Wataalamu pia wanatazama uwezekano wa kutumia dawa za majaribio kama remdesivir pamoja na dawa ya kingamwili ya MBP134 ambayo imeonyesha mafanikio katika majaribio ya wanyama. WHO pamoja na watafiti wa Chuo Kikuu cha Oxford wanasema majaribio ya kliniki yanaweza kuanza hivi karibuni katika maeneo yaliyoathirika ikiwa serikali za Kongo na Uganda zitatoa idhini.

Kwa sasa, mamlaka za afya zinaendelea kutoa tahadhari kwa wananchi kuhusu njia za kujikinga, hasa wakati wa kushughulikia wagonjwa au maiti za waliokufa. Ebola huenea kupitia majimaji ya mwili kama damu, matapishi au shahawa, na inaweza kuwa hatari sana wakati wa mazishi.

Wakazi wa Bunia na maeneo mengine yaliyoathirika wameeleza hofu yao huku wakikumbuka milipuko ya zamani ya Ebola iliyoua maelfu ya watu Afrika Magharibi zaidi ya muongo mmoja uliopita. Serikali ya Kongo sasa inasisitiza kuwa kuvunja mnyororo wa maambukizi ndiyo silaha muhimu zaidi kwa sasa wakati dunia ikiendelea kusaka chanjo na tiba ya kudhibiti mlipuko huo mpya.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW