Makombora ya Korea Kaskazini yazidi kuitisha Japan
8 Agosti 2017Japan kupitia katika waraka huo wa kila mwaka unaohusiana na masuala ya ulinzi uliotolewa Jumanne imetoa onyo juu ya kitisho cha Korea Kaskazini kinachotokana na mipango yake ya silaha za nyukilia.
Licha ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa vilivyowekwa dhidi ya nchi hiyo Korea Kaskazini imeendeleza majaribio yake ya makombora ikiwa ni pamoja na kufyatua makombora mawili ya kutoka bara moja kwenda jingine mwezi uliopita ambayo yalifika katika kisiwa cha Hokkaido magharibi mwa Japan.
Tangu mwaka jana wakati Korea Kaskazini ilipofanya majaribio mawili ya makombora ya nyukilia na makombora mengine 20 ya masafa marefu kitisho dhidi ya usalama kinaonekana kuchukua sura mpya. Umesema waraka huo wa wizara ya ulinzi ya Japan wenye kurasa 563.
Inafikiriwa kuwa mpango wa silaha za nyukilia wa Korea Kaskazini tayari umepiga hatua kubwa na huenda taifa hilo likawa tayari na makombora ya kinyukilia.
Majaribio ya hivi karibuni yaliyofanywa na Korea Kaskazini kwa kufyatua makombora ya kutoka bara moja kwenda jingine yanaonesha kuwa makombora hayo yanaweza kufika umbali mrefu zaidi ya Japan na pia kufika Marekani.
Japan yachukua hatua za tahadhari
Kuongezeka kwa kitisho cha Korea Kaskazini kumeifanya Japan kuchukua hatua za tahadhari ikiwa ni pamoja na mazoezi kadhaa ili kujiweka tayari iwapo kutatokea shambulizi lolote.
Kufuatia hatua ya Korea Kaskazini kuendelea na majaribio yake ya makombora kundi la wabunge kutoka chama tawala nchini Japan likiongozwa na Itsunori Onodera aliyateuliwa kuwa waziri wa ulinzi Alhamisi iliyopita lilimtaka Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe mwezi Machi kufikiria juu ya kuchukua hatua za kushambulia maeneo ya maadui hatua ambayo hata hivyo itaonekana kuwa ni mwelekeo mpya katika sera nje za Japan kuhusiana na masuala ya ulinzi.
Wakati serikali ya sasa ya Japan katika miaka ya hivi karibuni imepitia upya katiba ya nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti yake ya ulinzi hajawahi kufikiria kuwa na ndege za kivita au makombora ya masafa ya kutosha yenye uwezo wa kusambulia mataifa mengine.
Aidha waraka huo uliotolewa na wizara ya ulinzi ya Japan unaelezea juu ya hatua ya China kuzidi kujiimarisha katika ukanda huo ikigusia idadi ya ndege za kivita za Japan kulinganisha na China huku kukiwa na uwezekano kuwa shughuli zinazohusiana na na masualaya ulinzi katika ukanda wa bahari pamoja na zile za anga zinaweza kuongezeka katika ukanda wa bahari ya Japan kuanzia sasa.
Mahusiano ya Japan na China yameoneka kuzorota katika miaka ya hivi karibuni kutokana na mzozo wa visiwa visivyokaliwa na watu katika bahari ya China mashariki.
Wakati huohuo Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson amewasili Bangkok Thailand hii leo akiwa na wito wa kuitaka nchi hiyo ya kifalme kusitisha mahuasiano yake ya kibiashara na Korea Kaskazini ikiwa ni hatua ya Marekani za kuwashawishi washirika wake kuunga mkono juhudi zake za kuitaka Korea Kaskazini kuachana na malengo yake ya kuwa na silaha za nyukilia.
Thailand ni moja ya nchi za kusini mashariki mwa Asia zilizo na ofisi za ubalozi wa Korea Kaskazini na ina mahusiano mazuri ya kibiashara na Korea Kaskazini.
Kwa mujibu wa Suzan Thornton ambaye ni afisa wa Marekani anayehusika na masuala ya mashariki mwa Asia Tilleson analenga kuishawishi Thailand kuyadhibiti makampuni ya Korea Kaskazini yaliyoko nchini humo yanayotumia nafasi hiyo kzid kujiimarisha kibiashara.
Mwandishi: Isaac Gamba
Mhariri: Iddi Ssessanga