Majeruhi katika kikosi cha Bayern sio ajali au bahati mbaya
19 Februari 2016Hayo ni kwa mujibu wa mmoja wa wanasayansi maarufu wa michezo nchini Ujerumani.
Lars Lienhard ni mmoja wa wanasayansi wakuu wa michezo barani Ulaya, anayeshughuka na mfumo wa neva mwilini, yaani kuupa mafunzo ubongo. Alisaidia kuiandaa timu ya Ujerumani iliyoshinda Kombe la Dunia 2014 na sasa anafanya kazi na wanariadha wa Ujerumani kabla ya Olimpiki mjini Rio de Janeiro. Ameitumia Bayern Munich kama mfano wa kinachoweza kufanyika wakati wachezaji wanarejea uwanjani haraka baada ya kupona majeraha.
Bayern itapambana na Juventus katika mchuano wa hatua ya 16 za mwisho ya Champions League mjini Turin Jumanne wiki ijayo huku kikosi cha Guardiola kikiwa na mapungufu makubwa kutokana na majeruhi. Holger Badstuber aliyeumia wiki iliyopita ni mchezaji wa 16 wa kikosi cha Bayern kilichojaa wachezaji nyota ambao wamejeruhiwa msimu huu huku Jerome Boateng na Javi Martinez pia wakiwa mkekani. Frank Ribery hajarejea uwanjani kutokana na maumivu ya paja aliyopata mwezi Desemba.
Guardiola anatetea vikali mbinu zake za mazoezi akisisitiza kuwa hawarakishi wachezaji wake kurejea kutoka mkekani, baada ya kupata shutuma kutoka kwa vyombo vya habari hapa Ujerumani.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP
Mhariri: Gakuba Daniel