1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majeshi ya Afrika yako tayari kuingia Gambia

19 Januari 2017

Majeshi Senegal yakiungwa mkono na mengine ya Afrika yameweka kambi katika  mpaka  na  Gambia baada ya rais Yahya Jammeh kukataa  kuachia  madaraka wakati huu ambapo akiendelea kutengwa na maafisa wa serikali yake

Senegal Soldaten
Picha: Getty Images/AFP/Seyllou

Mkuu wa majeshi wa rais  Jammeh amesema jeshi lake halitoingia katika mapambano wakati majeshi hayo ya kigeni yatakapoingia katika ardhi ya taifa hilo wakati huu ambapo pia rais wa Mauritania ameondoka mjini Gambia baada ya kushindwa jitihada za mwisho kuachia madaraka kwa hiari. Mkuu wa majeshi Ousman Badjie amenukuliwa na vyombo vya habari akiosema "Hatuwezi kujihusisha kijeshi". Akiuita kuwa ni mgogoro wa kisiasa.

Afisa huyo wa ngazi ya juu kabisa katika jeshi la Gambia aliongeza kusema hawawezi kuwaingiza wanajeshi wao katika mapigano yakupuuzi. Anawapenda watu wake, na kama wanajeshi wa Senegal wakiingia "tutasalia kama hivi", akionesha mikono juu kama ishara ya kusalimu amri.

Muda ya Jammeh madarakani umemalizika

Rais wa Gambia Yahya Jammeh akisisitiza jamboPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

Muda wa Jammeh umefikia kikomo usiku wa manane lakini bado amekaidi kuachia ofisi baada ya kushindwa na mpinzani wake Adama Barrow katika uchaguzi wa mwezi uliopita, na kuzusha mashinikizo ya kumataka aachie ngazi kutoka kwa mataifa ya Afrika Magharibi, baada ya wiki kadhaa za kushindwa kwa mazungumzo ya kidiplomasia.

Nigeria imepeleka majeshi na ndege za kivita Senegal, taifa ambalo jeshi lake kwa wakati huu limekusanyika katika mpaka wa Gambia. Mashuhuda wanasema hali ya utulivu imetawala usiku wa kuamkia leo katika mji mkuu wa Bajul, ingawa majeshi yametawanywa pia katika mitaa ya mji huo.

Baraza la usalama kujadili Gambia

Chanzo kimoja cha kidiplomasia kimesema baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana leo kuridhia takwa la Afrika Magharibi lenye kumtaka Jammeh kukabidhi madaraka. Lakini msemaji wa Jeshi la Senegal, Kanali Abdou Ndiaye aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba kama suluhu za kisiasa zikishindwa tutafanya operesheni za kijeshi nchini Gambia.

Baada ya mazungumzi yake na Rais Jammeh, mjini Banjul, ambayo amesema yanamatumaini ya kufikia suluhisho la amani la kisiasa mpatanishi Rais wa Mauritania Mohamed Ould Abdel Aziz amewasili mjini Dakar, ambako amekutana na Barrow, akiwa amepatiwa hifadhi, na vilevile rais wa Senegal Mack Sally. Hayo ni kwa mujibu wa radio moja binafsi nchini humo.

Naye mkuu wa kamati ya maandalizi ya kuapishwa kwa rais mteule Adama Barrow, James Gomez, hafla ambayo ilipaswa kufanyika katika uwanja mkuu mjini Banjul amesema  kwa hivi sasa hafla hiyo imeahirishwa. Rais wa Gambia mwenye umri wa miaka 51 alitangaza hali ya hatari hapo Jumanne, iliofuatiwa na taarifa kuwa bunge limemruhusu kubakia madarakani kwa miezi mitatu .

Makamu wake wa rais Isatou Njie-Saidy amejiuzulu, sambamba na mawaziri  kadhaa  na mkuu wa jeshi la polisi kuacha utiifu, ikiwa ni katika tukio la karibuni la kujitenga na Rais Jammeh.

Mwandishi: Sudi Mnette

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW