Maalfu ya raia wanaswa katika mapigano
30 Mei 2016Kwa mujibu wa taarifa,majeshi ya Irak yameshaingia katika mji wa Fallujah na milio ya risasi ilikuwa inarindima.
Kamanda wa kikosi kinachopambana na ugaidi, Raji ameeleza kwamba majeshi ya kupambana na magaidi yalianza operesheni saa 11 alfajiri ya kuukomboa mji wa Fallujah.Amesema majeshi hayo yanasonga mbele na Mungu akipenda yataendelea na mafanikio.
Kamanda mwengine pia ameeleza kwamba majeshi ya Irak yanazidi kusonga mbele baada ya kuingia katika mji huo. Vikosi maalumu vya Irak vilikamilisha matayarisho ya mwisho hapo jana ili kuingia Fallujah.
Mapambano yanaendelea
Majeshi ya Irak yalianza mashambulio makubwa wiki iliyopita huku yakiungwa mkono na ndege za nchi zilizofungamana dhidi ya magaidi wanaojiita Dola la Kiislamu.
Makamanda wa majeshi ya Irak wamesema mapigano yanaendelea na wanatumai kuukomboa mji wa Fallujah katika muda wa siku chache zijazo.
Kamanda Thamir amesema majeshi ya serikali yameshakomboa asilimia 80 ya maeneo yanayouzunguka mji huo tangu kuanza kwa operesheni wiki iliyopita. Kamanda mwengine Yahya Rasoul amesema majeshi ya serikali yanasonga mbele vizuri na kwamba matokeo ya mapambano yatatangazwa mnamo saa zijazo.
Wakati huo huo vijiji kadhaa vinavyoizunguka ngome ya magaidi wa Dola la Kiilsamu vimekombolewa mapema leo.
Raia wanaswa katika mapigano
Umoja wa Mataifa umearifu kwamba maalfu ya raia wamenaswa katika mji Fallujah na mahitaji muhimu ya kila siku yameadimika. Kwa mujibu wa taarifa watu zaidi ya watu 50,000 wamekwama.
Mji wa Fallujah ulikuwa miongoni mwa miji muhimu ya kwanza ya Irak kutekwa na magaidi wa Dola la Kiislamu mwaka uliopita kutokana na mgogoro wa kisiasa nchini Iraq kuidhoofisha serikali.
Serikali ya Waziri mkuu Nuri al- Maliki iliamrisha msako wa Wasuni waliokuwa wanafanya maandamano . Miezi sita baadae wapiganaji wa Dola la Kiislamu waliingia kaskazini kwa Irak kwa kupitia kwenye maeneo ya Wasuni, na kuuchukua mji wa Mosul vile vile ,ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini Irak.
Katika kadhia nyingine bomu lililotegwa ndani ya gari lililipuka sokoni, katika kitongoji cha Washia kaskazini mwa mji mkuu Baghdad. Watu wasiopungua 20 wameuawa. Wengine zaidi ya 40 walijeruhiwa kutokana na shambulio hilo.
Shambulio hilo limefanyika muda mfupi tu baada ya majeshi ya Irak kuanza juhudi za kuukomboa mji wa Fallujah.
Mpaka sasa hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na shambulio hilo.Lakini kundi la Dola la Kiislamu aghlabu limedai kuhusika na mashambulio kama hayo.
Mwandishi: Mtullya Abdu.ape,rtre,
Mhariri: Mohammed Khelef