Majeshi ya Israel na Lebanon yapigana mpakani.
4 Agosti 2010Shambulio hilo linaelezwa kuwa baya kuwahi kutokea tangu vita vya mwaka 2006 kati ya Israel na wapiganaji wa Hezbollah na tayari jumuia ya kimataifa imetoa kauli kuhusiana na mapigano hayo.
Katika mapigano hayo wanajeshi wawili na mwandishi wa habari wa Lebanon waliuawa pamoja na afisa mwandamizi wa jeshi la Israel.
Pande zote mbili zilikuwa zikilaumiana kuchochea mapigano hayo, ambayo Lebanon imesema watu 15 wamejeruhiwa.
Mapigano hayo yalianzia katika kijiji cha Adaysseh na kuendelea kwa takriban saa nne.
Lebanon imesema imepeleka malalamiko katika baraza la Usalama la Umoja wa mataifa, ambalo wanachama wake wamekutana kwa faragha kwa mashauriano juu ya tukio hilo.
Baraza hilo la Umoja wa Mataifa pia limeelezea kusikitishwa kwake na mapigano hayo na kuzitaka pande hizo mbili kuwa na uvumilivu na kuzuia kuendelea zaidi kwa hali hiyo.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ambaye anafanya ziara nchini Japan, kupitia msemaji wake Martin Nesirky ameelezea pia kusikitishwa na tukio hilo na amezitaka pande hizo mbili kuonesha uvumilivu mkubwa na kushirikiana na umoja huo kuchukua hatua kuimarisha utulivu uliokuwepo sasa katika eneo hilo.
Umoja wa Ulaya na Marekani nazo pia zimezitaka nchi hizo mbili kujizuia na hali hiyo.
Mjini Washington, msemaji wa wizara ya mambo ya ncvhi za nje wa Marekani Philip Crowley ameelezea wasiwasi wake juu ya ghasia hizo na kuelezea masikitiko yao kwa wale wote waliopoteza maisha katika mapigano hayo.
Mjini Brussels, mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton amezitaka pande hizo mbili kuwa wavumilivu.
Kwa upande wake Waziri mkuu wa Lebanon Saad Hariri ambaye yupo nchini Italia amewataka viongozi mbalimbali wa dunia kujadili kile alichokiita uchokozi wa Israel.
Ameutaka Umoja wa Mataifa na jumuia ya kimataifa kuishinikiza Israel kuacha uchokozi wake.
Naye Mkuu wa baraza la usalama la Lebanon Jenerali Said Eid, kufuatia mkutano wa dharura ulioitishwa, amesema baraza hilo limetoa maelekezo ya kukabiliana kwa njia yoyote ile na uchokozi dhidi ya eneo lao, jeshi na watu.
Jeshi la Lebanon limesema wanajeshi walifyatua risasi baada ya wanajeshi wa Israel waliokuwa wakipiga doria kuvuka mpaka wa senyenge uliowekwa mpakani.
Israel nayo imejibu shutuma hizo dhidi yake kwa kusema kuwa serikali ya Lebanon inawajibika kwa tukio hilo.
Jeshi la Israel limesema majeshi ya Lebanon yalianza kuwafyatulia risasi wanajeshi wa nchi hiyo ndani ya ardhi yao.
Hali ya wasiwasi katika eneo hilo imekuwa ikiongezeka katika siku za hivi karibuni kufuatia ripoti kwamba kundi la wapiganaji la Hezbollah limekuwa likilimbikiza silaha kwa matayarisho ya kuanza vita vipya.
Kufuatia mapigano hayo kati ya wanajeshi wa Israel na Lebanon, Kiongozi wa kundi hilo la Hezbollah, Sheikh Hassan Nasrallah amewataka wafuasi wake kutojibu chochote, lakini amesema kundi hilo halitakaa pembeni katika siku zijazo.
Mwandishi: Halima Nyanza(afp)
Mhariri: Sekione Kitojo.